NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, ametoa wito kwa wadau wa elimu nchini kuunga mkono juhudi za serikali kwa kufadhili masomo ya elimu ya juu kwa wasichana hasa wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Prof. Mushi ametoa kauli hiyo leo Mei 29, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Shirika lisilo la Kiserikali la CAMFED Tanzania, unaolenga kujadili masuala ya ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu. Mkutano huo umehusisha wawakilishi kutoka vyuo vikuu 56 nchini.

Akipongeza juhudi za CAMFED, Prof. Mushi amesema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha idadi ya wasichana wanaonufaika na elimu inaongezeka, jambo linalochangia kuleta usawa wa kijinsia katika elimu.

Amesisitiza pia haja ya CAMFED kushughulikia changamoto ndogo ndogo zinazowakwamisha wanafunzi wa kike kupata ufadhili kwa urahisi. Miongoni mwa changamoto alizozitaja ni pamoja na masharti ya usajili chuoni yanayohitaji mwanafunzi awe amelipa ada kabla ya kusajiliwa.

"Suala la usajili wa wanafunzi limekuwa na changamoto ambapo mwanafunzi analazimika kuwa amelipa ada ili asajiliwe. Hili linapaswa kuangaliwa upya ili kuondoa vikwazo kwa wanafunzi wa kike. Pia, maendeleo ya wanafunzi wanufaika yafuatiliwe ili kuhakikisha fedha za ufadhili hazipotei bure," amesema Prof. Mushi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CAMFED Tanzania, Bi. Nasikiwa Duke, amesema lengo kuu la taasisi hiyo ni kusaidia watoto wa kike kutatua changamoto zinazoweza kuwazuia kumaliza elimu yao au kufikia ndoto zao.

Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa CAMFED Tanzania miaka 19 iliyopita, jumla ya wanafunzi 156,201 wamenufaika na ufadhili wa elimu kuanzia sekondari hadi shule ya upili.

"Kwa mwaka huu pekee, tumefadhili wanafunzi 36,424 kutoka shule 493 wanaosoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita," amesema Nasikiwa.

Katika elimu ya ufundi, CAMFED imefadhili wanafunzi 217 wanaosoma katika vyuo vya VETA na FDC, vilivyoko katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa upande wa elimu ya juu, amesema wanafunzi 6,302 wamefikiwa na ufadhili, ambapo kwa mwaka wa masomo wa sasa, wanafunzi 576 wanasoma katika vyuo mbalimbali 67 nchini.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...