WADAU wa usalama wa barabarani wametoa wito wa kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kudhibiti ajali za barabarani, wakisisitiza kuwa vifo na majeruhi vinavyotokana na ajali hizo hususani kwa Watoto, haviwezi kuvumilika tena katika jamii ya Watanzania.
Mwito huo umeungwa mkono leo Mei 29,2025 jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Miundombinu, Rogatus Mativila wakati wa uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya usalama barabarani katika Shule ya Msingi Sinza Maalum uliofanywa na Shirika la Amend Tanzania.
“Ajali za barabarani zimeendelea kuleta huzuni kwa jamii, hasa pale watoto wanapopoteza maisha au kujeruhiwa katika mazingira ya shule. Hili si jambo la kawaida tena. Ni wakati muafaka sasa kama taifa kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kupambana na janga hili,” amesema.
Ameongeza serikali kupitia TAMISEMI itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha shule zinakuwa maeneo salama kwa watoto, hasa kwa kuhakikisha uwepo wa vivuko vya watembea kwa miguu, matuta ya kupunguza mwendo, na alama za barabarani katika maeneo ya shule.
Aidha, alisisitiza kuwa watoto ni rasilimali muhimu ya taifa na kwamba ni lazima jamii yote ijikite katika kuhakikisha wanatembea kwa usalama kwenda na kutoka shuleni kila siku.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Amend Tanzania, Simon Kalolo alisema mradi huo ni wa kipekee kwa kuwa ni mara ya kwanza kutekelezwa kwenye shule yenye wanafunzi wenye mahitaji maalum pekee.
“Kwa zaidi ya miaka 13 ya kufanya kazi kwenye sekta ya usalama barabarani, hatujawahi kutekeleza mradi kwenye shule yenye watoto wa aina hii peke yake. Tunafahamu changamoto wanazokutana nazo, na tunaamini maboresho haya si tu yatapunguza ajali, bali pia yatatia moyo kwa wazazi kupeleka watoto shuleni,” amesema.
Ameongeza ajali za barabarani husababisha vifo vinavyokadiriwa kufikia milioni 1.3 duniani kila mwaka, huku wengine zaidi ya milioni 50 wakijeruhiwa, na kuwa chanzo kikuu cha vifo vya watoto na vijana wenye umri wa miaka mitano hadi 29.
“Tanzania na Afrika kwa ujumla vina iwango vya juu vya vifo barabarani licha ya kuwa na magari machache. Hili linaonyesha ni kwa kiasi gani tunapaswa kuchukua hatua za dharura,” amesisitiza.
Amefafanua mradi huo wa Amend umefikia shule 59 nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya ya shule 100 Afrika na kunufaisha wanafunzi zaidi ya 52,793 nchini Tanzania na zaidi ya 102,000 Afrika.
Wakati huo huo Mwakilishi wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani, SSP Mbunja Matibu amesisitiza jeshi hilo linaendelea kutoa elimu ya usalama kwa watoto na watu wazima, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na jamii.
“Tunatoa elimu mashuleni kwa watoto namna ya kuvuka barabara kwa usalama. Lakini pia tunahimiza watu wazima kuwavusha watoto, na abiria kuwajibika kwa kuwasimamia madereva wanaovunja sheria,” alisema Matibu.
Kwa upande wa Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia Elimu, Abedi Milanzi amesema maboresho hayo yamepunguza adha kubwa kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya FIA Foundation, Saul Billingsley ameeleza kwamba ameona miradi mingi ya Amend katika nchi mbalimbali Afrika na amevutiwa na dhamira ya shirika hilo kuwalinda watoto dhidi ya ajali.
Awali Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge alisema tatizo la ajali limekuwa kubwa Kinondoni na kutolea mfano Hospitali ya Mwanyamala kuwa imekuwa ikipokea watu wawili waliopoteza maisha kila siku kutokana na ajali hali ambayo ni sawa na vifo 60 kwa mwezi.
Katika Shule ya Msingi Sinza Maalum, miundombinu iliyowekwa ni pamoja na matuta ya kupunguza mwendo kasi, vivuko vya watembea kwa miguu, alama za barabarani, na njia maalum za watembea kwa miguu















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...