Na Mwandishi Maalum, Mtwara
SERIKALI kupitia Wizara ya Maji,imetoa Sh.815,453,185 ili kukarabati mradi wa Maji Dihimba utakaohudumia wakazi zaidi 7,489 wa Vijiji vya Dihimba,Mpondomo,Kinyamu na Ndumbwe vilivyopo Halmashauri ya Wilaya Mtwara Mkoani Mtwara.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike alisema,kati ya fedha hizo Sh.694,271,895 zimetumika kulipa Mkandarasi na Sh.121,181,200 zimetumika kwa ajili ya kununua bomba na Ruwasa Makao Makuu kwa kumtumia Mkandarasi M/S Zonghi Plumbing&General Supplies Company Ltd.

amesema,mradi huo ulianza kufanyiwa ukarabati Mwezi Januari 2024 na ulitakiwa kukamilika Mwezi Septemba, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa malipo ya hati ya madai na mvua nyingi umeshindwa kukamilika kwa muda,hivyo uliongezwa muda na utakamilika Mwezi Juni Mwaka huu.

Mashindike amesema,mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi M/S Seba Construction umefikia asilimia 75 na Mkandarasi amelipwa malipo ya awali kiasi cha Sh.100,766,635.90 na ulianzishwa ili kusogeza huduma ya majisafi na salama kwa Wananchi wa Vijiji hivyo na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya Mtwara.

Alisema,ukarabati huo umehusisha ujenzi wa tenki moja la lita 100,000 katika kijiji cha Mpondomo,ukarabati wa matenki mawili ya lita 200,000 katika Kijiji cha Ndumbwe na ujenzi wa vituo 17 vya kuchotea maji.

Alitaja kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba ya muhudumu,ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO),ununuzi na ulazaji wa bomba za maji umbali wa kilometa 9.74 zilizonunuliwa na Mkandarasi na ulazaji wa bomba umbali wa kilometa 14.781 zilizoletwa na Ruwasa Makao Makuu.

Kwa mujibu wa Mashindike,faida zilizopatikana kutokana na mradi huo ni pamoja na kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa Wananchi kutoka asilimia 37.04 ya awali hadi asilimia 93.47 mwaka 2025 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 56.43.

“Faida nyingine zilizopatikana ni kutatua changamoto ya maji iliyokuwepo katika vijiji vya Dihimba na Mpondo,Kinyamu na Ndumbwe,kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko katika jamii yanayotokana na matumizi ya maji yasio safi na salama,kuchochea maendeo na umetoa ajira za muda mfupi na mrefu kwa baadhi ya Wananchi”alisema.

Alieleza kuwa,mradi umezingatia sera ya maji ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuzingatia umbali usiozidi mita 400 kutoka kituo kimoja cha kuchotea maji kwenda kingine na hadi sasa jumla ya kaya 48,taasisi 2 za umma zimeunganishiwa maji na vituo 12 vipya vya kuchotea maji vimejengwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Patrick Sawala alisema,mradi wa maji Dihimba ulizinduliwa mwaka 1989, lakini tangu wakati huo haujafanyiwa ukarabati wowote hivyo ulishindwa kutoa maji ya kutoshelezaji mahitaji ya Wananchi wa vijiji husika.

Alisema,kutokana na changamoto hiyo Serikali imeamua kutoa fedha ili kukarabati mradi huo ambao sasa umewezesha wananchi kupata huduma ya majisafi na salama na kupunguza muda kwa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao.

Alisema,katika Mkoa wa Mtwara kuna miradi mikubwa na midogo ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mradi wa Maji wa Miji 28 wa Mto Ruvuma unaotarajiwa kupeleka maji katika Mji wa Mangaka,Masasi na Nachingwea Mkoa jirani wa Lindi.

Alisema,miradi hiyo ikikamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 71 maeneo ya Vijijini hadi asilimia 85 ifikapo mwaka 2030 ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ili kuwaondolea Wananchi changamoto ya majisafi na salama.

Mkazi wa Kijiji cha Dihimba Mwanahawa Rashid alisema,kabla ya ukarabati huo walitembea kilometa 2 hadi 3 kila siku kwenda vijiji vya jirani kutafuta maji kwa kuwa katika kijiji chao kulikuwa na bomba moja tu lililojengwa kupitia mradi wa Jaica ambalo halikutosheleza kutoa maji ya uhakika.

“Tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya sita iliyofanikisha kukarabati mradi wa maji katika Kijiji chetu cha Dihimba,nawapongeza watendaji wa Ruwasa kusimamia vizuri mradi ambao umetusaidia sana kupata maji ya uhakika”alisema.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara Mhandisi Hamis Mashindike aliyeshika fimbo,akimuonyesha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi miundombinu ya mradi wa maji Dihimba uliofanyiwa ukarabati mkubwa ili kuboresha hduma ya majisafi na salama kwa Wananchi wa Vijiji vinne vya Dihimba,Mpondomo, Kinyamu na Ndumbwe.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akiangalia kisima cha maji katika kilichofanyiwa ukarabati mkubwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa Wananchi wa Vijiji vya Ndumbwe,Dihimba,Mpondomo na Kinyamu Wilayani Mtwara,kushoto Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike na kulia Mkuu wa Wilaya hiyo Abdala Mwaipaya.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara Hamis Mashindike kushoto,akitoa maelezo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kuhusu ukarabati wa Mradi wa Maji Dihimba unaohudumia zaidi ya Wakazi 7,489 wa vijiji vinne Wilayani Mtwara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...