UBALOZI wa Tanzania nchini Sweden umeratibu ushiriki wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira duniani unaofanyika tarehe kuanzia leo tarehe 7 hadi 8 Mei, 2025, jijini Copenhagen nchini Denmark.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Masauni, ambapo mawaziri 30 wanaosimamia masuala ya mazingira kutoka katika mataifa mbalimbali, Kamisheni ya Umoja ya Ulaya na wadau wengine wa mazingira wameshiriki.
Lengo la mkutano huo ni kupokea taarifa ya kila nchi ya namna ilivyochangia katika kupunguza gesi joto duniani, kubadilishana uzoefu na kuweka mipango ya maandalizi ya mkutano wa COP 30 unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2025 nchini Brazil.
Ajenda ya Tanzania katika mkutano huo ni kuongeza upatikanaji wa fedha katika utekelezaji wa programu za mabadiliko ya tabianchi, nishati safi ya kupikia na kuhakikisha kuwa fedha zilizokuwa zimeahidiwa na wafadhili mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo zinatolewa kwa wakati.
Ajenda nyingine ni kushawishi wadau wa mazingira kutoa misaada yenye masharti nafuu ya kutekeleza programu za mazingira na kuwekeza katika teknolojia ya upimaji wa hewa ya kaboni ikiwa ni pamoja na kujengea uwezo taasisi zinazoratibu masuala ya mazingira nchini.
Kwa upande mwingine, Tanzania imeeleza nia yake ya kuendelea kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa njia ya ubia na kwa kutumia rasilimali zake za asili kama vile bahari, misitu, madini adimu, maziwa, mito pamoja na ujenzi wa miundombinu rafiki kwa mazingira.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...