Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Peres Magiri,akizungumza na baadhi ya Wajasiriamali wadogo kutoka kata mbalimbali Wilayani humo ambao wamekidhi vigezo vya kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya Nyasa,kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Khalif.
Baadhi ya Wajasiriamali wadogo kutoka Kata mbalimbali za Wilaya ya Nyasa wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Peres Magiri(hayupo Pichani)wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya vikundi vilivyokidhi vigezo kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma Khalid Khalif,akitoa taarifa ya mikopo ya asilimia 10 inayotoewa na Serikali kwa makundi maalum ya Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu ambapo Halmashauri hiyo imetenga zaidi ya Sh.milioni 300 kukopesha makundi hayo.

Mwandishi Wetu, Nyasa
HALMASHAURI ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma,kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imetenga kiasi cha Sh.319,831,500 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Kati ya fedha hizo Sh.217,000,0000 zimetolewa katika robo ya pili ambapo Sh. 86,800,000 sawa na asilimia 40 zilitengwa kwa ajili ya wanawake,Sh. 86,800,000 kwa vijana na Sh.43,000,000 sawa na asilimia 20 kwa watu wenye ulemavu.


Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Khalif,kwenye hafla fupi ya kutoa vyeti kwa vikundi 20 vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo isiyo na riba iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri Wilayani Nyasa.


Khalif alisema,baada ya fedha hizo kutangazwa Sh.189,831,500 zilitolewa kwa vikundi 39 ikiwemo vikundi 17 vya wanawake vimepata Sh.milioni 86,800,000,vikundi 11 vya vijana vimepata Sh.72,090,000 na vikundi 11 vya watu wenye ulemavu vilivyopata Sh.30,941,000 kati ya Sh.43,400,000 iliyotangazwa.


Kwa mujibu wa Khalif,katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri imetenga na kutangaza kiasi cha Sh.130,000,000 kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kati ya hizo Sh.41,132,600 sawa na asilimia 40 zitatolewa kwa wanawake.



Alisema Sh.55,842,100 sawa na asilimia 40 ikujumlishwa na Sh.14,709,500 iliyobaki katika robo ya pili zitatolewa kwa vijana na watu wenye ulemavu wametengewa Sh.33,025,300 sawa na asilimia 20 ikujumlishwa na Sh.12,459,000 iliyobaki katika robo ya pili.



Aidha alisema, Halmashauri ya Wilaya Nyasa itatoa mikopo yenye thamani ya Sh.107,474,000 kwa vikundi 20 ikiwemo vikundi 9 vya wanawake,7 vikundi vya vijana na 4 kwa watu wenye ulemavu huku Sh.21,526,000 zimesalia kutoka katika fungu la watu wenye ulemavu kutokana na kundi hilo kujitokeza watu wachache walioomba mkopo.


Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri alisema kuwa,mikopo hiyo ni agizo la kisheria linalotaka kila Halmashauri hapa nchini kutenga asilimia 10 yatokanayo na mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha makundi maalum ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.


Amewataka walengwa,kwenda kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili watu wengine wenye sifa waweze kukopeshwa kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.



Alisema,mpango mpya wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu utaimarisha usalama wa fedha za Serikali huku akisisitiza walengwa kuhakikisha wanafanya marejesho kwa wakati.


Magiri alisema,miaka ya nyuma utoaji wa mikopo kupitia Halmashauri za Wilaya ulikumbwa na changamoto nyingi hususani katika urejeshaji wa mikopo kwani wajasiriamali walijiunga kwenye vikundi lakini walishindwa kudumisha biashara zao,hivyo kukumbwa na madeni makubwa yaliyoathiri maisha yao.


Mbunge wa Jimbo la Nyasa Stella Manyanya,amewapongeza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Khalid Khalif kwa kazi kubwa ya kukusanya mapato yake ya ndani yaliyofanikisha kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi hayo.


Amewapongeza baadhi ya wanawanchi waliamua kuanzisha biashara ambazo zimewezesha kuwa na sifa ya kupata mikopo na kusisitiza kwenda kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kununua nguo au kwa wanaume kuongeza idadi ya wanawake.


“huu ni mkopo unaotakiwa kurejeshwa na sio zawadi,nategemea kuona Nyasa inayoendelea kupiga hatua kubwa kiuchumi kupitia mikopo hii inayotolewa na Halmashauri yetu,mkatumie vizuri fedha hizi ili ziweze kuwaondolea umaskini”alisema Manyanya.


Mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo Imakulatha Challe kutoka kikundi cha Twaweza kata ya Linga kinachojishughulisha na ufugaji wa kuku,ameishukuru Serikali kwa kutoa mikopo ambayo itasaidia kuimarisha biashara zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...