WATAYARISHAJI wa filamu kutoka Nchini Tanzania, Kefa Hussein Igilo na Jerryson Onasaa, wameipeperusha vyema bendera ya taifa baada ya kushinda tuzo kubwa katika hafla ya 11 ya utoaji wa Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA) iliyofanyika usiku wa kuamkia Mei 10, 2025, jijini Lagos, Nigeria.

Kazi yao ya kipekee Wa Milele – tamthilia ya maisha ya uhalisia (reality series) iliyodhaminiwa na Showmax – imeibuka mshindi katika kipengele cha Tamthilia Bora ya Uhalisia Barani Afrika (Best Unscripted Series), ikiwapiku washindani wengine wanne kutoka Nigeria.

Tuzo hiyo ya heshima ilitolewa na Bi. Fahmeeda Cassim Surtee, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji (Group) wa DStv Media Sales pamoja na Dkt. Eno Udoma-Eniang, Mkurugenzi wa Masuala ya Mahusiano ya Kampuni na IDF.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Kefa Igilo alisema, “Hii ni tuzo ya Watanzania wote. Tunatoa shukrani za dhati kwa MultiChoice Tanzania kwa kuamini uwezo wetu, na pia kwa Shirika la Utangazaji Tanzania kwa ushirikiano wao wa karibu. Tunatambua na kuunga mkono jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuinua tasnia ya filamu nchini. Ushindi huu ni ushahidi kuwa Tanzania inaweza.”

Wa Milele? ni kipindi cha maisha halisi kinachochunguza ndoa nne zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali. Wanandoa hao huwekwa pamoja katika jumba moja kwa muda wa mwezi mzima, wakijadili matatizo yao hadharani, wakielimisha na kuibua mjadala mpana kuhusu maisha ya ndoa katika jamii ya sasa. Mwishoni mwa kipindi, kila wanandoa hufikia uamuzi wa kuendelea au kuvunja ndoa yao.

Tuzo za AMVCA ni miongoni mwa tuzo kubwa na zenye heshima zaidi barani Afrika katika sekta ya filamu na runinga, zikikusanya kazi bora kutoka kila kona ya bara. Ushindi wa Kefa na Jerryson unathibitisha ukuaji mkubwa wa tasnia ya filamu nchini Tanzania na mchango wa vipaji vya vijana katika kusukuma mbele mipaka ya ubunifu wa Kiafrika.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...