Dar es Salaam: Katika kuendelea kudhihirisha dhamira yake ya muda mrefu katika kuimarisha afya ya umma, Benki ya Exim Tanzania, kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), imefanikisha kampeni ya nchi nzima ya uchangiaji damu. Zoezi hili muhimu, lililofanyika katika vituo saba (7) kote nchini ikiwemo Dar es Salaam (Makao Makuu Exim Tower na Kaburi Moja), Dodoma (Veta na Kizota), Mtwara, Kahama na Mbeya, linaimarisha msaada thabiti wa benki kwa NBTS katika kukabiliana na upungufu wa damu nchini.
Kama sehemu ya juhudi za mwaka huu, Benki ya Exim pia imekabidhi jumla ya vifaa 110 muhimu vya kimatibabu kwa NBTS. Vifaa hivi muhimu vinalenga kuimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa NBTS wa kukusanya na kuhifadhi damu nchi nzima, na hatimaye kuongeza ubora, usalama na upatikanaji wa damu katika vituo vya afya vya umma kote Tanzania.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bi. Kauthar D’souza, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, alisisitiza, “Tunajivunia kuongoza zoezi hili muhimu la uchangiaji damu, tukiendeshwa na kaulimbiu yetu 'Changia damu na okoa maisha'. Mpango huu ni nguzo muhimu ya programu yetu pana ya 'Exim Cares', ambapo benki yetu inashirikiana kikamilifu na jamii si tu katika afya, bali pia katika sekta za elimu, uendelevu wa mazingira, kukuza uvumbuzi, na uwezeshaji kiuchumi. Ushirikiano wetu wa kudumu na NBTS kwa zaidi ya miaka 10 unaonesha imani yetu dhabiti kwamba kila mchango wa damu ni kitendo muhimu, kinachookoa maisha ya mtu fulani mahali fulani nchini Tanzania.”
Bi. D’souza aliongeza, "Huu ni mpango wa kitaifa wa uchangiaji damu, sio tu Dar es Salaam, bali unafanyika katika jumla ya maeneo saba katika ikiwemo Dodoma, Mtwara, Kahama na Mbeya kwa wakati mmoja, kwa lengo la kuongeza kiasi cha damu itakayokusanywa ikilinganishwa na mwaka jana."
Kwa upande mwingine, Bi. Judith Charle, Msimamizi wa Huduma za Wachangia Damu kutoka NBTS, alielezea shukrani zake za dhati kwa ushirikiano huu unaoendelea. “Tunashukuru sana kwa msaada na ushirikiano na Benki ya Exim kwa miaka mingi sasa. Ushirikiano wao ni muhimu katika kutusaidia kuziba pengo la upatikanaji wa damu kwani tunaamini kila damu inayokusanywa, na kila kifaa kinachotolewa, kinamaanisha moja kwa moja maisha ya Mtanzania yanaokolewa mahali fulani.”
Kampeni hii ya uchangiaji damu inajengwa juu ya mafanikio ya kampeni za awali za damu zilizofanywa na Benki ya Exim kwa kushirikiana na NBTS. Kampeni ya mwaka huu iliyopanuliwa inalenga kufikia watu wengi zaidi na kuhamasisha uwajibikaji mkubwa wa kiraia miongoni mwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Tanzania inalenga kukusanya takriban chupa 550,000 vya damu kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya nchi kwa asilimia 100. Ingawa NBTS inajitahidi kukusanya chupa 350,000 za damu kila mwaka, bado idadi hii iko chini ya mahitaji yote. Changamoto hii inazidishwa na ukweli kwamba takriban asilimia 15 ya damu iliyokusanywa huwa haiwezi kutumika kutokana na sababu mbalimbali, jambo linalosisitiza hitaji la haraka la michango zaidi.
Zaidi ya sekta ya afya, Benki ya Exim inaunga mkono kikamilifu mipango ya jamii na serikali katika maeneo mbalimbali. Hii ni pamoja na uwekezaji muhimu katika elimu, mazingira, uundaji wa ajira, na kukuza uvumbuzi. Mfano wa hivi karibuni wa dhamira hii ni mchango wa benki wa madarasa mawili mapya yenye samani kwa shule mbili katika wilaya ya Buhigwe, mkoa wa Kigoma, mapema mwaka huu.
Benki ya Exim Tanzania inasalia kuwa mshirika thabiti katika maendeleo ya kitaifa, ikiwekeza daima si tu katika ujumuishaji wa kifedha na uvumbuzi, bali pia katika sekta muhimu kama afya, elimu, na ustawi mpana wa jamii.
MWISHO
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...