Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Beno Malisa ametoa hamasa kwa Wafanyabiashara Mkoani Mbeya kuhakikisha kuwa wanakua na utamaduni mzuri wa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuweza kutatua kero mbalimbali zinazohusu masuala ya kodi.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kuanza kwa Kampeni ya utoaji elimu ya kodi ya mlango kwa mlango Wilayani hapo yenye lengo la kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanaelimishwa kiuhusu kodi, wanatatuliwa kero zao za kikodi na kujengewa mazingira mazuri ya kulipa kodi.
Ameongeza kuwa, ulipaji kodi unaleta manufaa kwa Taifa kwa kuleta maendeleo mbalimbali nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo, Afya, Elimu bure, Ujenzi wa Miundombinu mbalimbali, hivyo wafanyabiashara hawanabudi kulipa kodi zao stahiki kwa wakati.
“Nichukue fursa hii kuwaomba wafanyabiashara wote mtakaotembelewa katika maeneo yenu katika zoezi hili kutoa ushirikiano kwa Maafisa wa TRA ili muweze kuwasilisha changamoto zenu na ziweze kutatuliwa”, alisema Malisa.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Uhusiano wa TRA, Bw. Hudson Kamoga amesema kuwa, lengo la kampeni hiyo pia ni kuhakikisha kwamba utatuzi wa changamoto zinazowakabili walipakodi kwa mwezi huu wa Juni zinatatuliwa kikamilifu.
Kwa upande wao Wafanyabiashara wa Soko la SIDO Mkoani hapo wamepongeza zoezi la kupatiwa elimu ya mlango kwa mlango na kuomba liwe endelevu kwasababu linawasaidia kutatua changamoto zao za kikodi.
Kempeni ya elimu kwa Mlipakodi ya mlango kwa mlango ni zoezi endelevu ambalo TRA imekua ikiliendesha nchi nzima kwa kuhakikisha kwamba, Wafanyabiashara wanapewa elimu ya kodi na kukumubushwa haki na wajibu wao katika masuala ya kodi ambapo kwa sasa zoezi hilo lipo mkoani Mbeya na litaendelea kwa Mkoa wa Njombe.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...