Na Diana Byera-Bukoba


Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imeadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda miti 500 ya matunda katika Hospitali ya Wilaya.

Akifungua zoezi hilo, Dr. Kisanga Makigo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, alihimiza taasisi na watu binafsi kuendelea kupanda miti ili kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tumeamua kuchagua eneo hili la hospitali kwani lina uhitaji wa miti ya vivuli na matunda ili kuleta mwonekano na uboreshaji wa mazingira haya yanayotoa huduma za afya. Tunaamini kuwa baadhi ya miti iliyopandwa itakuwa msaada mkubwa katika kulinda mazingira yetu lakini pia itasaidia jamii inayotuzunguka kupata matunda,” alisema Makigo.

Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Dominic Ruta, alieleza kuwa miti zaidi ya 500 imepandwa, ikijumuisha miparachichi, michenza na miti ya kivuli. Alisisitiza kuwa zoezi hili ni endelevu katika taasisi zote za serikali na binafsi kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza lishe.

Alisema kuwa halmashauri hiyo kupitia Idara ya Mazingira itaendelea kusambaza miti mingine ya aina tofauti hadi ngazi ya kaya ili kujenga jamii bora inayolinda mazingira, huku zoezi hilo likiwahusisha hata watoto wanaoendelea kukua.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya, Elizeus Ezra, alishukuru halmashauri kwa kuchagua kupanda miti katika hospitali hiyo mpya, akibainisha kuwa watumishi na wagonjwa watanufaika kwa kupata matunda na kuwepo kwa mandhari tofauti hospitalini hapo.

Aidha, alishukuru wadau wote wa afya wa Bukoba Vijijini na nje ya Bukoba wanaoendeleza juhudi za kuboresha mazingira hospitalini hapo na kudai kuwa miti hiyo itatunzwa kama kumbukumbu bora ya Siku ya Mazingira Duniani ya mwaka huu.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni, ambapo kwa mwaka huu inaongozwa na kaulimbiu isemayo:

"Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki."








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...