Wilaya ya Ubungo inatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru Alhamisi, tarehe 5 Juni 2025, ukitokea Wilaya ya Kinondoni, ambapo mapokezi yatafanyika katika stendi ya Kibamba kuanzia saa 12:00 asubuhi. Mwenge huo utakimbizwa umbali wa takribani kilomita 72 ukitembelea miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 8.2.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, miradi hiyo inajumuisha sekta za Elimu, Afya, Maji, Barabara, Maendeleo ya Jamii, Usafi na Mazingira. Mwenge wa Uhuru utazindua, utakagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha maendeleo ya jamii.
Mbali na shughuli za maendeleo, Mwenge wa Uhuru pia utatumika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakaofanyika mwezi Oktoba, chini ya kaulimbiu “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani na utulivu.”
Katika mkesha wa Mwenge, ambao utafanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Makuburi kuanzia saa 10:00 jioni, kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Harmonize na Dullah Makabila. Aidha, huduma za bure za upimaji wa afya kama vile VVU, malaria na magonjwa mengine zitatolewa kwa wananchi.
Wananchi wa Ubungo wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi, kushuhudia miradi, na kusherehekea mwenge huo wa kitaifa. Mwenge wa Uhuru utakabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuukabidhi Mkoa wa Tanga siku ya Ijumaa, tarehe 6 Juni 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...