Na Philomena Mbirika, Dodoma
Kufuatia maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya utalii kwa wananchi pamoja na wadau wa utalii waliotembelea banda NCAA lililopo kwenye Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa mingine waliofika kwenye banda la NCAA wanapata elimu na ufahamu juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na NCAA kwenye Utalii, Uhifadhi na Maendeleo ya jamii huku wengi wakionekana kuvutiwa zaidi na vivutio vya Utalii vinavyopatikana Hifadhi ya Ngorongoro kama Bonde la kreta ya Ngorongoro, nyayo za Laitole, bonde la Olduvai George, Kreta ya Empakai, Mchanga unaohama na vivutio vingine.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Utalii kutoka idara ya Huduma za Utalii na Masoko, Joseph Mzaga alieleza kuwa maadhimisho hayo ya wiki ya utumishi wa umma yamewakutanisha na wadau mbalimbali na imekuwa fursa kwao kutangaza vivutio vya utalii ambako wananchi wameonekana kuwa na shauku ya kutembelea hifadhini hapo.
“Tumepokea wageni mbalimbali walioweza kufika kwenye banda letu ambao wengi wao walitamani kufahamu zaidi kuhusiana vivutio vya utalii, namna ya kufika hifadhini, viingilio na taarifa zingine Muhimu za kuwasaidia kwa ajili ya maandalizi ya safari zao “ Alisema Mzaga.
Kwa upande wake, Bi. Agatha Antony ambaye ni mkazi wa Mkoa wa Dodoma aliyetembelea banda la NCAA alieleza kuwa maonesho hayo yamekuwa msaada mkubwa kwake na wenzake wanaopanga kutembelea Ngorongoro, kwa kuwa wamepata taarifa muhimu kuhusu gharama za kuingia hifadhini, njia za usafiri, na mambo ya kuzingatia kabla ya safari, jambo ambalo litawasaidia kujipanga vizuri na kuongeza hamasa kwao.
“Mimi pamoja na wafanyakazi wenzangu kutoka taasisi ya Pharma Afrika tunajiandaa na safari ya kutembelea hifadhi yaa Ngorongoro na leo nimefurahi zaidi kwani nimeweza kufika hapa na nimepata taarifa ambazo zitatusaidia kwenye maandalizi yetu mfano viingilio, usafiri na vivutio ambavyo tutaweza kuvitembelea.” Alisema Agatha.
Wiki ya utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa watumishi wa Umma katika maendeleo ya Taifa ambapo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Himiza Matumizi ya Mfumo wa Kidijitali Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji”.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...