
Makamu wa Rais wa Huaxin Group (mwenye koti) Wang Jiajun akiongoza watendaji wengine katika uzinduzi rasmi wa cement mpya ya Newta Jijini Dar es Salaam
*Kampuni ya Maweni Limestone Ltd (MLL-Tanzania), tanzu ya Huaxin Group, yazindua saruji mpya ya Newta,
KAMPUNI ya Maweni Limestone Ltd (MLL-Tanzania), ambayo ni kampuni tanzu ya Huaxin Group, imezindua bidhaa mpya ya saruji ijulikanayo kama Newta, ambayo inalenga kuleta mageuzi chanya katika sekta ya ujenzi nchini Tanzania.
Uzinduzi huu unakuja wakati miradi mingi ya maendeleo na ujenzi ikiendelea kutekelezwa nchini, ambapo hitaji la bidhaa bora na za kisasa linazidi kuongezeka.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika leo Juni 17, 2025 jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Huaxin Group, Wang Jiajun, alisema kuwa uzinduzi wa Newta umetokana na utafiti wa kina uliofanywa na kampuni hiyo ili kuhakikisha inazalisha bidhaa bora itakayokidhi mahitaji ya soko la ndani.
"Matokeo ya utafiti wetu yameleta bidhaa ya ubora wa hali ya juu inayofaa kwa matumizi ya mafundi wapya na wakongwe. Saruji hii mpya inarahisisha kazi na inatoa matokeo bora katika umaliziaji wa miradi ya ujenzi," alisema Jiajun.
Aliongeza kuwa Newta ina faida nyingi, ikiwemo uwezo wa kukauka haraka, jambo litakalowezesha wakandarasi na mafundi kuokoa muda na kuendelea kwa kasi katika hatua nyingine za ujenzi. Aidha, muonekano wake wa kuvutia unafanya majengo kuwa na mvuto wa kipekee.
Jiajun aliwataka wadau wa sekta ya ujenzi kuchangamkia fursa zitakazotokana na bidhaa hiyo mpya, huku akieleza kuwa saruji hiyo inazalishwa katika kiwanda cha Mkuranga mkoani Pwani, na kwamba mipango ya usambazaji nchi nzima iko tayari kupitia mtandao madhubuti wa usafirishaji wa kampuni hiyo.
"Tuna imani kuwa Watanzania wataipokea vyema Newta, ambayo ni matokeo ya jitihada za uongozi wetu kuhakikisha tunaleta ubunifu na ubora katika sekta ya ujenzi," alisema.
Akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Jiajun alisema kuwa mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali ndiyo yaliyowezesha kampuni yao kuwekeza kwa mafanikio hapa nchini.
"Tanzania imekuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji kwa kampuni yetu, ambayo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa saruji duniani. Tuna viwanda viwili — kimoja Mkuranga, Pwani na kingine Tanga — ambavyo vina uwezo mkubwa wa uzalishaji," alifafanua.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa MLL, Louis Liu, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Huaxin Group kwa ngazi ya kimataifa, Jessica Ma, mawakala wa biashara, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi.
Huaxin Group, iliyoanzishwa mwaka 1907 nchini China, ni moja ya kampuni kubwa zaidi duniani katika uzalishaji wa vifaa vya ujenzi, na kupitia kampuni zake tanzu zaidi ya 300, inaendesha shughuli katika zaidi ya nchi 18. Kampuni hiyo ilianza uwekezaji wake rasmi Tanzania mwaka 2019.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...