Puma Energy Tanzania imedhihirisha kujizatiti kwake katika kukuza sekta ya usafiri wa anga nchini kwa kudhamini Mkutano wa Wadau wa Ukuaji wa Sekta ya Anga Afrika mwaka 2025 unaojulikana kama AviaDev Africa, uliofanyika kuanzia tarehe 11 mpaka 13, Juni, katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.


Kupitia hotuba yake wakati wa tafrija ya jioni iliyohudhuriwa na viongozi na wadau wa anga kutoka kote barani Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah, alielezea mchango wa kimkakati wa kampuni hiyo katika maendeleo endelevu ya sekta ya anga nchini Tanzania.

“Usafiri wa anga ni kiungo muhimu cha maendeleo ya taifa,” alisema Bi. Abdallah. “Kama msambazaji pekee wa AvGas na mtoa huduma mkuu wa mafuta ya Jet A-1 nchini Tanzania, Puma Energy Tanzania inajivunia kuwa mshirika wa kuaminika katika kuchochea uunganishwaji wa anga, utalii na biashara.”

Alibainisha uwepo mpana wa Puma Energy Tanzania katika zaidi ya viwanja vya ndege nane muhimu, vikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro, na Uwanja wa Abeid Amani Karume. Uwekezaji wa hivi karibuni katika miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi mafuta, mifumo ya kisasa ya kuhifadhia maji, na malori ya kujaza mafuta yaliyo na teknolojia ya hali ya juu, umeongeza ufanisi wa uendeshaji na usalama, na kuiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati kama kitovu cha anga katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Bi. Abdallah alisisitiza mchango mpana wa kampuni hiyo kwa uchumi—ikiwemo kutoa ajira katika sekta ya usafirishaji na uhandisi, kusaidia sekta ya utalii yenye thamani zaidi ya Dola bilioni 3, pamoja na kuwezesha biashara ya kimataifa kupitia huduma bora za kujaza mafuta kwa ndege za mizigo.

Aliihakikishia hadhira dhamira ya Puma Energy Tanzania katika kuhakikisha usalama na uendelevu, akieleza kuwa kampuni inazingatia viwango vya IATA, ICAO, na JIG, sambamba na kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira ili kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.

“Hatujioni kama wasambazaji wa mafuta tu, bali kama pia marubani wa maendeleo—washirika katika kujenga mfumo wa usafiri wa anga ulio imara, endelevu, na unaounganisha dunia kwa mfumo wa anga,” alihitimisha.

Katika kipindi cha siku tatu za mkutano (Juni 11–13), wadau muhimu wa sekta za anga na utalii walijadili mada kama vile ushirikiano wa wadau, uhusiano baina ya maeneo ya utalii na mashirika ya ndege, mageuzi ya sera, matumizi ya akili mnembe (AI) katika anga, upangaji wa mitandao ya safari, na ukuaji wa mapato yasiyotokana na usafirishaji wa abiria.

Majadiliano na warsha zililenga changamoto na fursa katika kuunganisha Afrika kwa njia ya anga, fedha za usafiri wa anga, upatikanaji wa masoko, uimara wa bima, na njia ambazo bado hazijahudumiwa, zikiendeleza ushirikiano na mikakati bunifu.

Mkutano huo uliwakutanisha wadau muhimu wakiwemo Puma Energy Tanzania, AviaDev, Tume ya Utalii Zanzibar, Zanzibar Presidential Delivery Bureau (ZPDB), Proflight Zambia, Flightlink, Fastjet, Air Tanzania, Ethiopian Airlines, Kenya Airways, TAAG Angola Airlines, Embraer Commercial Aviation, AFRAA, Ravinala Airports, Mamlaka ya Utalii Ghana, Baraza la Biashara la SADC, Serikali ya Western Cape, Jetcraft Commercial Limited, na TrueNoord, miongoni mwa wengineo.

Kwa kuhitimisha, Bi. Abdallah ana matumaini makubwa siku zijazo, akielezea dira ya Puma Energy Tanzania:

“Tukiwa tunahudumia ndege kila baada ya dakika mbili katika mabara manne tofauti duniani, mchango wetu mkubwa zaidi uko Afrika. Natoa wito kwa wadau tuwekeze kwenye mustakabali wa fursa, ubunifu, na uunganishwaji.”





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...