Na Diana Byera – Simiyu
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetangaza mpango wa kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), hatua inayolenga kurahisisha na kuboresha uratibu wa shughuli za wafugaji nchini.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji, alitoa kauli hiyo mbele ya maelfu ya wafugaji katika Uwanja wa Kabindi, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, alipokuwa akijibu maombi ya wafugaji waliotaka kupatiwa kiwanja kwa ajili ya kujenga ofisi za chama chao.
Waziri Kijaji alieleza kuwa kiwanja hicho kitapatikana mkoani Dodoma na kitakuwa maalum kwa shughuli za uratibu wa sekta ya mifugo, ikiwemo utambuzi wa wafugaji kwa njia ya kidijitali.
“Serikali iko katika hatua za mwisho za kupata hati miliki ya eneo hilo, ambalo litatumiwa na CCWT kusimamia na kushughulikia changamoto mbalimbali za wafugaji nchini,” alisema Dkt. Kijaji.
Akieleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika sekta ya mifugo, Waziri huyo alisema kuwa tayari serikali imesambaza tani 105 za mbegu za malisho, kugawa madume kwa wafugaji 408 na kujenga majosho 754 katika kipindi cha miaka minne.
Aidha, serikali imeendelea kuweka miundombinu wezeshi kwa wawekezaji wa ndani kujenga viwanda vya kuchakata nyama na maziwa, sambamba na kupunguza tozo kwa wanaoingiza vifaa hivyo, hatua ambayo imesaidia kuongeza soko la kudumu kwa wafugaji, na hivyo kuchangia kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Waziri Kijaji amegawa vifaa vya kilimo kwa wafugaji wanaolima malisho ya mifugo na kuzindua televisheni maalumu ya mifugo, ambayo itakuwa ikitoa maudhui ya kielimu na ujuzi wa kisasa kuhusu ufugaji bora.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCWT, Mrida Mshota, alisema chama hicho kimesajili wafugaji 22,000 kwa njia ya kidijitali hadi sasa, huku lengo likiwa ni kufikia wafugaji milioni 4 ifikapo mwaka 2030! amemuomba Waziri Kijaji kusaidia jitihada za kuanzisha benki ya mifugo kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wafugaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...