Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
VIONGOZI na wanachama  wa taasisi ya  uwezeshaji  wa wanawake  kiuchumi Tanzania  TAWEN  wametakiwa kuwekeza  elimu kwa mtoto wa kike  kwa sababu elimu ni silaha  ya kwanza  ya kumuwezesha  mwanamke  kusimama , kujisimamia  na kuongoza  kwa ujasiri  na weledi.

"Sambamba na hilo  ili tuweze kufikia  malengo hayo   tunayoyatarajia  hatuna  budi  kwa umoja  wetu  sote  kupambana  na kupinga  vitendo  vya ukatili  kwa watoto  hususan  kipindi hiki  ambacho  kinaripoti matukio  mengi ya ukatili  kwa watoto kama kubakwa, kulawitiwa, ndoa za  utotoni, mimba za utotoni, familia kutelekeza  watoto , ajira  za watoto na watoto wengi  kukosa haki  ya kupata elimu".

Hayo yamesema na  Afisa Utumishi Mwandamizi   Shirika la Elimu Kibaha  Mkoani Pwani  Emmanuel Lweyo alipokuwa mgeni rasmi katika mafunzo ya uongozi kwa wanachama  wa  Taasisi   ya Uwezeshaji  wa Wanawake  Kiuchumi  Tanzania (TAWEN) iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Sports Lounge Kibaha Mkoani Pwani tarehe 9 Juni 2025.

Lweyo amesema kuwa ni muhimu  kuwa na mazingira  rafiki  kwa wanawake  anaotaka  kuingia kwenye uongozi  ikiwemo sera  zinzolinda  haki zao  nafasi  za uwakilishi  wa lazima na kuondoa ubaguzi wa kijinsia.

"Jamii zetu lazima zibadilike  mtazamo  wa kwamba  mwanamke  hawezi  kuwa kiongozi huu ni mzigo  wa fikra  potofu  ambao tunapaswa kuuangusha  kwa nguvu  ya elimu, mazungumzo ya wazi na mfano bora  kutoka  kwa wanawake  waliopiga hatua  na mfano  mzuri  kwa nchi yetu ni Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan , Spika wa Bunge la Tanzania  na Spika wa  Mabunge  Duniani Mhe. Dkt. Tulia Ackson na wengine  waliopata nafasi  za juu  za uongozi  wa taifa letu" amesema Lweyo.

"Katika historia  ya jamii  nyingi  wanawake  wamekuwa  wakionekana  kama wapishi  wa familia  walezi wa watoto na wasaidizi  wa waume zao  lakini  ukweli  ni kwamba  wanawake  ni zaidi  ya hayo, mwanamke  ana uwezo  wa kuongoza  ,kupanga, kuamua na kuleta  mabadiliko  makubwa  katika  familia , jamii, taifa  na hata  dunia kwa ujujmla"amesema Lweyo.

Katika dunia ya leo hatuwezi  tena  kuzungumzia  maendeleo  bila kuhusisha  wanawake , hatuwezi  tena  kupanga sera  kuendesha  siasa  au kusimamia uchumi  kwa mafanikio  bila  ushiriki  wa kina   wa wanawake katika  nafasi  za uongozi.

Lweyo amesisitiza kwa kusema kuwa "tunahitaji wanawake katika  nyanja  za  kisasa katika  bodi  za mashirika  kwenye  uongozi  wa shule  , taasisi za kifedha  na kwenye nyanja zote za maisha"amesema Lweyo.

Akimnukuu Hayati Nelson Mandela " Elimu  ni silaha  yenye  nguvu  zaidi  unavyoweza  kuitumia  kubadilisha dunia" tukimpa  mwanamke elimu  na nafasi  ya kuongoza  tutakuwa  tumebadilisha  dunia si kwa maneno  bali kwa vitendo.
 Kwa hiyo leo tunapozungumza  juu ya mustakabali  wa taifa  letu  tusisahau  kwamba maendeleo  ya kweli  hayaji  bila  usawa  wa kijinsia , kukuza uongozi  wa wanawake  si hisani  ni haki , si chaguo ni wajibu  na siyo kwa faida ya wanawake pekee  bali kwa faida ya  ya kizazi chote.

Taifa linalothamini  na kujali  ndoto  na makuzi  ya watoto  ndilo taifa  hai kwa  kuwa  watoto  ndiyo nguvukazi , viongozi  na wabeba maono  ya taifa  la baadaye  hivyo  ni wajibu  wetu sote  kuwalea  katika maadili mema kuwalinda  na kuwapatia  haki zao  za msingi  ili tupate  Taifa lililo bora.

Viongozi wengine  wa TAWEN  waliohudhuria mafunzo hayo ni  Mwenyekiti Florence Masunga , Katibu Dafroza Mzava,  Afisa Miradi Asha Baraka Mwenyekiti wa Vijana TAWEN Cosmas Ikwabe na Mwenyekiti wa Umoja Wa Wanawake Wilaya ya Kibaha (UWT) Mwajuma Nyamka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...