Na Janeth Raphael MichuziTv

Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma katika Wizara ya Fedha, Dkt. Frederick Mwakibinga amesema mnyororo wa ugavi ni moja ya nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa na kusisitiza kuwa usimamizi hafifu katika hatua yoyote ya mnyororo huo unaweza kusababisha hasara kwa Serikali na kuwanyima wananchi huduma stahiki.

Dkt. Frederick Mwakibinga ameyazungumza hayo leo Mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari na wamiliki wa mitandao ya kijamii yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha,

Dkt. Mwakibinga amesema kuwa mnyororo wa ugavi unaanzia katika upangaji wa mahitaji, ununuzi, ugomboaji, upokeaji, uhifadhi, usambazaji, matumizi hadi uondoaji wa bidhaa, vifaa au huduma.

“Kwa kutumia kalamu zenu, sauti, picha na majukwaa yenu ya habari, tunaamini elimu kuhusu nafasi ya mnyororo wa ugavi katika maendeleo ya taifa itawafikia wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesisitiza Dkt. Mwakibinga.

Kwa upande wake Mathias Canal ambaye ni Mwenyekiti wa Waandishi wa Habari na Wamiliki wa vyombo vya habari vya Mitandao ya Kijamii wanaoandika habari za Wizara ya Fedha, ameipongeza Wizara hiyo kwa kuendelea kutoa elimu kwa waandishi wa habari, kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu seta mbalimbali zilizopo chini ya Wizara ya Fedha,

Aidha Canal amesema kuwa hatua hiyo itaongeza uelewa utakaowaimarisha katika utoaji taarifa katika jamii kuhusu matumizi ya fedha za umma.

"Kwa kupitia mafunzo haya, uelewa wa umma utaongezeka na pia utahamasisha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi," Amesisitiza Bw Canal.

Naye,Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, amesema kuwa ushirikiano kati ya Wizara na vyombo vya habari umeendelea kuimarika, na kuahidi kuwa Wizara itaendelea kuandaa mafunzo zaidi kwa ajili ya kuwawezesha wanahabari kuelewa kwa kina sera, mipango na shughuli za Serikali.

“Mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Fedha kuelimisha umma kuhusu sera, programu na matukio mbalimbali ya maendeleo kupitia vyombo vya habari,” alisema Bw. Mwaipaja.

Awali akiwasilisha mada kuhusu Mnyororo wa Ugavi, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt. Maige Mwasimba, amesema kuwepo kwa mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa shughuli za mnyororo wa ugavi kunasaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali, kuimarisha ubora wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha mnyororo huo unatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika kwa maendeleo endelevu.

“Faida ya kuwa na mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini ni pamoja na kuwezesha ukusanyaji wa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mwenendo wa usambazaji wa bidhaa, utendaji wa wahusika mbalimbali, na changamoto zinazojitokeza katika kila hatua ya ugavi,” ameeleza Dkt.Maige.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...