Na mwandishi wetu,  DODOMA
WAZIRI wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewataka wananchi kulinda mazingira ya vyanzo vya maji kwa kuacha kukata miti ovyo na kufanya shughuli za kibinadamu ili kuepuka ukame.

Ametoa wito huo mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 2, 2025 yanayoendelea kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Mhe. Aweso amesema kuwa uwepo kwa rasilimali za maji toshelevu ni usalama wa taifa kwakuwa uwepo wa maji ni uhakika wa chakula, nishati ya umeme pamoja na mipango ya kimaendeleo ambapo yote hayo yanategemea na mazingira endelevu.

Pia, Waziri Aweso alisema ni wakati sasa Watanzania watambue kuwa athari za mazingira ziwe funzo, akitolea mfano Mto Ruvu mkoani Pwani ulivyokauka kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yalisababishwa na binadamu wenyewe.

“Athari za mazingira ziko wazi kwa mfano ukienda Pangani athari zikio wazi, leo tunaona bahari imekula mji na hivyo kina cha maji kinaongezeka kina kwahiyo changamoto hizi za kimazingira tunazoziona sasa ziwe funzo kwetu,” alisema.

Pamoja na changamoto hizo, alishukuru na kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mikakati thabiti na hatua madhubuti inazochukua katika kuyasimamia na kuyatunza mazingira.

Amesema hayo yote yanafanyika kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa kusimamia agenda ya mazingira.

“Nashukuru kwa kupata nafasi ya kutembelea mabanda haya, hakika Ofisi ya Makamu wa Rais mmejipanga na sisi kama Wizara ya Maji tutaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuyalinda na kuyatunza mazingira ili kuhakikisha Tanzania inakuwa bora na salama, kama mtakumbuka tumefanya mabadiliko ya Sera ili yaendane na mazingira,” alisema Mhe. Aweso.

Maonesho hayo ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 5, 2025 ambayo itakuwa kilele chake.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...