-Asisitiza dhamira ya Serikali kuwainua wachimbaji wadogo kiuchumi

-Mitambo Yagharimu shilingi bilioni 12.41

-STAMICO yasaini mkataba wa ushirikiano na VETA

Dodoma,

Katika mwendelezo hatua za Serikali kuendelea ya kuimarisha sekta ya wachimbaji wadogo nchini, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezindua rasmi mitambo 10 ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo yenye thamani ya shilingi bilioni 12.41 iliyonunuliwa na Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) sambamba na vitendea kazi vya Shirika hilo kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Shirika.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo Juni 24, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa madini, wachimbaji pamoja na wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuwawezesha wachimbaji wadogo ili wainuke kiuchumi na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa pato la taifa pamoja na kukuza vipato vyao binafsi.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ndiyo maana Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 imeelekeza kuwasaidia kwa kuwatengea maeneo, kuwawezesha kufanya utafiti, kuwapatia mitambo ya uchorongaji na uchimbaji wa madini kwa njia za kisasa,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha kuwa mitambo hiyo 10 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 12.41 ni mwendelezo wa juhudi zilizowekwa na Serikali ambapo Rais alizindua mitambo mitano Oktoba 2023 ambayo tayari imeanza kutumika na kutoa mchango mkubwa kwa wachimbaji. Kupitia mitambo hiyo, wachimbaji wadogo wameanza kuaminiwa na taasisi za kifedha, hivyo kuongeza uwezo wao wa kukopesheka.

Aidha, amesema mitambo miwili kati ya hiyo 10 imetengwa mahususi kwa ajili ya kuwahudumia wanawake wachimbaji, ikiwa ni sehemu ya kujumuisha jinsia zote katika fursa za kiuchumi kupitia sekta ya madini.

Katika tukio hilo, pia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini mkataba rasmi wa ushirikiano na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ili kuhakikisha watumuaji wa mitambo hiyo ya kisasa wanajifunza matumizi sahihi na ya kitaalamu kuendesha mitambo hiyo.

Mhe. Majaliwa amepongeza juhudi za STAMICO na kuwataka wachimbaji kuhakikisha wanauza madini yao katika viwanda vya kusafisha dhahabu na kwenye masoko rasmi ili kukomesha biashara haramu na utoroshaji wa madini.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa masoko 43 ya madini na vituo 109 vya ununuzi, ili kuleta mazingira bora ya kibiashara na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata masoko yenye uhakika.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kuwa tukio hilo ni ushuhuda wa namna Shirika hilo lilivyopiga hatua katika miaka ya karibu, na kuanza kujitegemea sambamba na kutoa gawio Serikalini.

“Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na usimamizi wake wa Sekta ya Madini ambao leo umetufikisha hapa, mbali ya kununua mitambo hii, STAMICO pia inajenga kiwanda kikubwa cha kuchakata Madini ya Chumvi Wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi, hatua itakayowasaidia wakulima wa chumvi kupata soko la uhakika na bei nzuri” amesisitiza Mavunde.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa uzinduzi wa mitambo hiyo na vitendea kazi ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuhakikisha Shirika la Madini la Taifa linafanya shughuli zake kwa tija zaidi, huku wachimbaji wadogo wakinufaika moja kwa moja na uwepo wa shirika hilo kama mlezi wa kundi hilo muhimu.

“Mhe. Waziri Mkuu, Mitambo hii ya uchorongaji (drilling rigs) uliyozindua leo, ina faida nyingi kwa wachimbaji wadogo, hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia hii inaleta mabadiliko makubwa katika utafutaji na uchimbaji wa madini kwa ufanisi na usalama zaidi. Ikiwemo, Kuboresha Utafiti wa Madini ambapo huwasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa kina na kupata taarifa sahihi kuhusu tabaka la ardhi na uwepo wa madini kabla ya kuanza kuchimba kiholela. Hii huongeza nafasi ya kugundua mashapo ya madini yenye tija.” Amesisitiza Dkt. Mwasse.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...