*Ni baada ya wawekezaji na wafanyabiashara kuonesha nia ya kuwekeza nchini

UWEPO wa miundombinu bora na imara ni miongoni mwa vitu muhimu vinavyohitajika katika kuliwezesha taifa lolote duniani kupata maendeleo ya kiuchumi yanayowawezesha wananchi wake kujikwamua kutoka katika wimbi la umasikini.

Katika kuhakikisha Taifa linakuwa na miundombinu bora na yenye kutosheleza mahitaji Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imejipanga kuhakikisha inaboresha sekta ya miundombinu.

Mbali na sekta ya miundombinu pia Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuimarisha sekta zingine za kimkakati zikiwemo za kilimo, afya, nishati na real estate kupitia miradi ya PPP lengo likiwa ni kukuza uchumi.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kikazi nchini Japan pamoja na mambo mengine ziara hiyo ililenga kukutana na viongozi na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa nchi hiyo na kuwashawishi kuja kuwekeza nchini.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kushawishi kampuni za Japan kushirikiana na Tanzania kuwekeza kimkakati katika sekta za kilimo, afya, uchumi wa buluu, nishati, miundombinu, ufugaji na TEHAMA ili kuweza kutoa ajira kwa Watanzania.

Miongoni mwa viongozi aliokutana ni pamoja na Waziri Mkuu wa Japan, Shigeru Ishiba ambaye alimuhakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano hayo.

Mheshimiwa Majaliwa alisema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo kuwa  pamoja na miradi mingine wanayotekeleza nchini, Japan kupitia JICA iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi ambayo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba alieleza kuridhishwa na uimarikaji wa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kuihakikishia Serikali ya Tanzania kwamba makampuni mbalimbali ya Japan yataendelea kufanyakazi nchini ili kusaidia katika kukuza uchumi, kuendelea masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu nchini inaendelea kuongezeka.

Kuhusu ombi la kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi, Mheshimiwa Ishiba aliwaelekeza viongozi wa JICA pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania Youichi Mikami kwenda kutembelea barabara hizo na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.


MKUTANO NA MAKAMU WA RAIS WA JICA

Jumatano, Mei 28, 2025, Waziri Mkuu alikutana na Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura ambaye alimuhakikishia kuwa shirika JICA itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.

Makamu huyo wa Rais wa JICA alisema hatua hiyo inatokana na namna ambavyo Serikali imekuwa ikisimamia kikamilifu matumizi ya fedha mbalimbali zinazotolewa na wadau wa maendeleo likiwemo shirika hilo. Baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa JICA ni pamoja na mradi wa Ustahimilivu wa Chakula (TSRP) na Tanzania Agricultural Inputs Support Project (TAISP).

Kwa upande wake, Waziri Mkuu alitoa wito kwa JICA kuendelea kutafuta wadau zaidi wa maendeleo kwa ajili upatikanaji wa fedha zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwafanya Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. “Serikali itaendelea kusimamia ipasavyo fedha zote za maendeleo zinazoletwa nchini na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.”

Amesema lengo la wito huo ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wanafungua milango ya kiuchumi ili wananchi wengi washiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kujiongezea kipato.

“Lengo la kutafuta wadau hawa ni kuwawezesha wananchi washiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi, wanaotaka kuingia kwenye biashara, wanaotaka kuingia kwenye kilimo, sekta ya madini, sekta ya uvuvi na ufugaji haya ni maeneo ambayo tumeyawekea umuhimu.”

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alitumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa JICA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 516 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kilimo.

Mheshimiwa Silinde alitaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Ustahimilivu wa Chakula (TSRP) unaogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 371 ambazo kati yake Benki ya Dunia imetoa Dola milioni 300.05 na JICA imetoa Dola milioni 71.09, ambapo utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.

Amesema mradi mwingine ni wa Tanzania Agricultural Inputs Support Project (TAISP) unaotekelezwa kwa ubia kati ya Benki ya Maendeleo Afrika na JICA unaohusika na utoaji wa ruzuku katika pembejeo za kilimo.

Naibu Waziri Shilinde amesema mradi huo unaotarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 145, ambapo kati ya fedha hizo, JICA wanatoa dola milioni 70 na AfDB dola milioni 75.49 na ulianza kutekelezwa mwaka 2024 na utakamilika 2028. Tayari dola milioni 40 zimelipwa kwa kampuni 17 kwa ajili ya usambazaji wa mbolea.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Ali Mohamed Ameir amesema katika vikao hivyo amewahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan uwepo wa mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yao Zanzibar ikiwemo hali ya amani na utulivu.

Pia, Mheshimiwa Ameir alitumia fursa hiyo kuiomba JICA kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukamilisha miradi miwili ya ujenzi ikiwemo upanuzi wa soko na jiko la samaki katika eneo la Malindi hususani kutoa vifaa kwa wafanyabiashara pamoja na mradi wa usambazaji maji mijini katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Miradi yote inatekelezwa kwa awamu ya pili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri ameishukuru Serikali ya Japan kupitia JICA kwa kugharamia washauri elekezi wawili ambao watakuwa kiungo kati ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na Tanzania.

Alisema washauri hao elekezi ambao watakuwepo TIC mmoja ni Mtanzania na mwingine Mjapani watakuwa na majukumu ya kutoa taarifa za namna ya kufanikisha uwekezaji kati ya Tanzania na Japan.

“Lengo la huyu mwelekezi kutoka Japan ni kuzungumza na kusaidia makampuni na wawekezaji kutoka Japan kupata taarifa za namna ya kuja kuwekeza Tanzania na huyu wa Tanzania ni kusaidia Watanzania wote wanaotaka kuuza bidhaa zao Japan.”


MKUTANO NA MAKAMPUNI MAKUBWA TOKYO

Jumatano, Mei 28, 2025 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu, Shirikisho la Wawekezaji na Wafanyabiashara nchini Japan (KEIDANREN) na Jumuiya ya Wamiliki, Marais na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Makampuni wa Japan (KEIZA DOYUKAI).

Alitumia fursa hiyo kueendelea kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Japan kuja kuwekeza kwenye sekta za kilimo, afya, uchumi wa buluu, nishati, miundombinu, ufugaji na TEHAMA kwani Serikali imeshaboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji.

“Tunakaribisha makampuni ya Japan kuchangamkia fursa nyingi za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania, zikiungwa mkono na mazingira tulivu ya biashara, mageuzi ya sera, na juhudi zinazoendelea za kupunguza urasimu.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa alikutana na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan (MLIT), Kenichi Ogasawara pamoja na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta za Miundombinu Japan na Afrika (JAIDA) Miyamoto Yaichi

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za MLIT na kuhudhuriwa na Marais wa makampuni makubwa ya uwekezaji ya Japan, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za nishati, miundombinu, utalii, kilimo na biashara.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa Tanzania imejiimarisha katika kujenga uwezo wa rasilimali watu, hivyo aliwakaribisha katika kutoa mafunzo na programu za kubadilishana maarifa zitakazowezesha wahandisi wa Kitanzania, wapangaji miji, na wataalamu wa miundombinu kunufaika na utaalamu na ubunifu mkubwa wa Japan.

Alisema Japan imeendelea kuwa mmoja wa washirika wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na kwa kipindi cha miaka mingi, nchi hizo mbili zimejenga uhusiano thabiti, hasa katika eneo la miundombinu. “Tunathamini sana uhusiano huu na mchango mkubwa wa makampuni ya Kijapani katika maendeleo ya Taifa letu.”

Alisema Serikali inaamini kuwa miundombinu bora ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuboresha maisha ya watu, kuwezesha biashara, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda. “Lengo la Tanzania kuendelea kuboresha mtandao wa barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege”.

“Haya ni maeneo muhimu ya kuimarisha muunganiko wa ndani ya nchi na maeneo ya kikanda. Miradi mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR) na upanuzi wa bandari za Dar es Salaam na Mtwara ni mifano thabiti ya dhamira yetu ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji wa kikanda.”

Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amesema kuwa ametumia vikao kuwaeleza wawekezaji na wafanyabaishara hao kuhusu mipango na mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inavutia zaidi uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Aidha, Mheshimiwa Nyongo amesema kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuwa na dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambayo itaeleza kwa kiasi kikubwa itasaidia kubainisha maeneo muhimu ya uwekezaji ili yanayolenga kukuza uchumi wa nchi.

Naye, Muwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNDP) Shigeki Komatsubara amesema kuwa Tanzania itaendelea kunufaika na utaalam na teknolojia kutoka Japan katika sekta mbalimbali zikiwemo za Miundombinu na Rasilimali watu.

 

Makala haya yametolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...