Na Said Mwishehe,Michuzi TV
KAMPENI maalum ya kutangaza vivutio vya utalii nchini iliyopewa jina la Tinga Chan,Tinga Tanzania imezinduliwa nchini ikiwa na lengo la kuhamasisha mashabiki wa soka barani Afrika kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania.
Kupitia kampeni ya Tinga Chan,Tinga Tanzania mashabiki wa soka mbali ya kushuhudia mechi mbalimbali katika michuano ya CHAN inayotarajiwa kuanza rasmi Agosti 2 mwaka huu katika Uwanja wa Makapa jijini Dar es Salaam pia watapata nafasi kutembelea vivutio vilivyopo nchini iwe Tanzania Bara au Zanzibar.
Akizungumza leo Julai 31,2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utali Tanzania(TTB) Ephraim Mafuru amesema bodi ya utalii imekuwa na majukwaa wanayotumia kutangaza utalii na katika michuano ya CHAN watatumia Jukwaa la michuano hiyo kutangaza vivutio vya utalii nchini na hivyo wamekuja na kampeni maalum ya Tinga Chan Tinga Tanzania.
“Bodi ya Utalii Tanzania tumekuja na kampeni ya maalum inaitwa TINGA CHAN ,TINGA TANZANIA malengo makubwa ni matatu ikiwemo kutangaza vivutio na upekee wa vivutio vya Utalii vilivyopo nchini Tanzania…
“Lakini kupitia matangazo ya michuano hii mtakubaliana nami kwamba unapoangalia zao hili la utalii wa michezo umeendelea kukua kwa kasi sana duniani.Kwahiyo bodi ya utalii imejidhatiti kutumia fursa ya nchi 19 kuwepo Tanzania kwa mwezi mzima hivyo mashabiki mbalimbali wa soka kutembelea vivutio vya utalii,”amesema Mafuru.
Akieleza zaidi amesema bodi ya utalii wokati wa michuano ya CHAN imedhamiria kuwapa fursa wageni ambao wanaingia katika nchini Tanzania kwenda kuona vivutio vya utalii .
“ Najua Watanzania wengi wamehamasika na watakuja viwanjani ,watakwenda kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii lakini wageni wanaokuja Tanzania tunajua mechi hazichezwi kila siku na hawawezi kwenda mechi zote.
“Hivyo wanapoangalia mechi moja moja na kati ya mechi na mechi waende kutembelea vivutio vya utalii kwani tunazo hifadhi za Taifa , tunamakumbusho ya Taifa.Tunayo maeneo ya burudani lakini tuna maeneo mbalimbali ambayo wanaweza kwenda kununua baadhi ya bidhaa ambazo ni za utalii.”
Ametoa mwito kwa Watanzania wageni wanapokuja wahudumiwe vizuri na kisha waende wakashuhudie vivutio na kusisitiza michuano ya CHAN pia inakuja na fursa za kiuchumi hivyo Watanzania wachangamkie ujio wa nchi 19 kwa ajili ya michuano hiyo.
“Tuichangamkie fursa hii ,kwa kushirikiana na Wizara ya Habari , Utamaduni,Sanaa na Michezo tumejidhatiti kuhakikisha kwamba fursa hii ya CHAN kuwa Tanzania iache alama katika kipato cha mtanzania mmoja mmoja, kipato kwa kampuni,kipato kwa nchi lakini kama Tanzania tumepata heshima ya kuandaa CHAN kwa mara ya kwanza na kuleta nchi 19 nchini .
“Kwa kipekee Bodi ya Utalii Tanzania tunatoa shukrani kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake mbalimbali ambazo zimewezesha michuano ya CHAN kufanya katika nchi za Tanzania ,Kenya na Uganda na ufunguzi utafanyika nchini Tanzania.”
Hata hivyo amesema bodi ya utalii wameamua kwamba michuano hiyo itafanyika Dar es Salaam na Zanzibar lakini kuna mikoa mingi yenye wapenzi wa mpira hivyo wameamua katika maeneo mbalimbali ya wazi mikoani ikiwemo Dar es Salaam ,Morogoro,Dodoma,Mbeya,Arusha na Mwanza kutakuwa na maeneo ambayo yataandaliwa kuangalia mechi live.Pia kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.
Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Rodney Thadeus, amesema maandalizi ya michuano hiyo yamekamilika kwa asilimia 100 hivyo kinachosubiriwa ni kuanza kwa michuano hiyo ambao amewakumbusha Watanzania kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ambako viingilio vitakuwa Sh.10,000, Sh.5000 na Sh.2000.
Amesema pia katika michuano hiyo mbali ya kushuhudia mechi katika Uwanja wa Mkapa pia kutakuwa na burudani ya muziki wa Singeli ambako kutakuwa na wana muziki wa singeli wote maarufu .
”Hivyo mashabiki wa soka wako wakimaliza kuangalia mpira wanashuka chini kuangalia Singeli.Tunawaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi.”amesema Thadeus na kusisitiza kuwa Kampeni ya Tinga Chan ,Tinga Tanzania imekuja wakati sahihi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...