Na Karama Kenyunko – Michuzi TV

KATIKA kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Vifo kwa Kuzama Duniani inayofanyika kila Julai 25, Shirika la Environmental Management and Economic Development Organisation (EMEDO) limezindua tuzo maalum kwa ajili ya kutambua mchango wa waandishi wa habari katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu usalama wa majini.

Uzinduzi huo umeenda sambamba na wito kutoka kwa wataalamu mbalimbali wakisisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi na za kitaifa kuhusu vifo vitokanavyo na kuzama ili kuelewa vyema ukubwa wa tatizo hilo na kupanga mikakati thabiti ya kukabiliana nalo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Julai 24,2025  Mjumbe wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Edwin Soko, alisema tuzo hizo, zitakazojulikana kama Water Safety Journalist Awards (WASA), ni njia ya kuenzi kazi za waandishi walioko mstari wa mbele katika kuripoti habari zinazohusu kuzuia vifo vya kuzama.

 "Tuzo hizi zitahusisha waandishi kutoka vyombo vyote—redio, magazeti, televisheni, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali. Lengo ni kuhamasisha uandishi wa habari wa kijamii wenye athari chanya na kuimarisha taaluma ya uandishi kwa maslahi ya umma," alisema Soko


Kwa mujibu wa EMEDO, kazi zitakazoshindanishwa zitapimwa kwa vigezo vya ubunifu, matumizi ya takwimu sahihi, athari katika jamii, na uelewa mpya kwa wasomaji au watazamaji. Kazi hizo zinapaswa kutumwa kupitia barua pepe awardsdp@gmail.com, zikifuatana na ushahidi wa kuchapishwa au kurushwa hewani.

Katika mkutano huo, Soko alisisitiza kuwa bila takwimu sahihi za kitaifa, ni vigumu kupima mafanikio ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau. Alieleza kuwa watu wengi hupoteza maisha kwa kuzama, hasa katika maeneo ya uvuvi na usafiri wa vyombo vya majini.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 236,000 hufariki kila mwaka duniani kutokana na kuzama, nusu yao wakiwa chini ya umri wa miaka 30. Katika Tanzania, wastani wa vifo ni 2.2 kwa kila watu 100,000, lakini katika maeneo ya wavuvi kama Ziwa Victoria kiwango kinapanda hadi 217 kwa kila watu 100,000, ambapo asilimia 87 ya vifo vya watu wazima vinahusiana moja kwa moja na uvuvi kwa kutumia mitumbwi.

Afisa wa Utetezi wa EMEDO, Mary Francis, alisisitiza kuwa ni wakati sasa kwa Tanzania kuwa na mfumo wake wa ukusanyaji wa takwimu badala ya kutegemea taarifa za kimataifa pekee.

 "Kwa sasa tunategemea sana takwimu za WHO, ambazo haziwezi kuakisi hali halisi nchini. Hili linapunguza ufanisi wa mipango yetu," alisema

Kaulimbiu ya mwaka huu ni: "Hadithi yako yaweza kuokoa maisha," ikiwa ni mwaliko kwa kila mmoja kutumia sauti yake kuhamasisha usalama wa majini.

Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Nyanda, alisema jeshi hilo linaunga mkono jitihada za EMEDO na limekuwa likitoa mafunzo ya vitendo na nadharia kwa jamii za wavuvi.

 "Tunafundisha mbinu za kuogelea na matumizi ya vifaa vya usalama kama maboya. Pia tunasisitiza utoaji wa taarifa za dharura mapema kwani kila sekunde ni muhimu katika uokoaji," alieleza Nyanda

Alitahadharisha kuwa baadhi ya watu hutumia namba za dharura vibaya kwa mzaha, hali inayoweza kuchelewesha msaada na kusababisha vifo.

Naye Sabina Hamis, mtaalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), alisema TMA inaendelea kutoa tahadhari na utabiri wa hali ya hewa kwa wakati ili kusaidia kupunguza ajali majini.

 "Tunafuatilia mabadiliko ya hali ya hewa na kutoa taarifa kwa taasisi na wananchi husika, hasa wavuvi na wasafiri wa majini," alisema.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...