Na mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dk. Moses Kusiluka anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo ya siku nne kwa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kuanzia Julai 28-31, 2025 katika shule ya uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani, yanaratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.
Lengo la mafunzo hayo kwa watendaji wakuu wapya na wale ambao hawajawahi kupatiwa mafunzo ni kuwajengea uwezo watendaji wakuu ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu Alhamisi, Julai 24, 2025, alisema Program ya mafunzo kwa watendaji wakuu ni kielelezo dhahiri cha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha kuwa watendaji wanajua nini wanatakiwa kwenda kufanya katika taasisi walizopewa kuongoza.
“Mafunzo haya yanayolenga kuongeza tija na ufanisi katika taasisi za umma, ni endelevu,” alisema Bw. Mchechu.
Ikumbukwe kwa mara ya kwanza mafunzo haya yalifanyika Oktoba 2024.
Bw. Mchechu alisema kuwa programu hiyo ya mafunzo ni mwendelezo wa hatua mbalimbali ambazo Ofisi ya Msajili wa Hazina inachukua katika kutafsiri na kutekeleza kwa vitendo maono ya Mheshimwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na falsafa ya 4Rs.
“Katika falsafa ya 4Rs tumejikita katika R mbili kati ya nne ambazo ni Reform (mabadiliko) na Rebuild (kujenga upya),” alisema.
Alifafanua: ”Hapa tutajikita zaidi katika eneo la kuwajengea uwezo watendaji wakuu ili wawe na ufanisi zaidi katika usimamizi wa taasisi za umma.”
Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi, mashirika ya umma, wakala wa serikali na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache 308, huku uwekezaji ukiwa n Sh86.25 trilioni.
Kati ya kiasi hicho Sh83.33 trilioni zimewekezwa kwenye taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali, huku Sh2.92 trilioni zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...