Na Belinda Joseph-Songea.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Songea Mkoani Ruvuma, imeibuka na ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya mkaa, ambapo imesisitiza kuwa Serikali haijapandisha bei ya zao hilo muhimu la misitu, bali imebadilisha utaratibu wa usafirishaji ili kulinda misitu ya nchi.
Akizungumza Meneja wa TFS Wilaya ya Songea Mhifadhi Issa Mlela, amesema kuwa Serikali haijazuia matumizi ya mkaa kwa wananchi, bali imeweka utaratibu rasmi wa kusafirisha mkaa kwa kutumia vyombo vya usafiri vyenye magurudumu manne au matatu (gari au guta), badala ya bodaboda kama ilivyokuwa awali, hatua inayolenga kudhibiti uharibifu wa misitu na kuhakikisha mkaa unaopatikana unatokana na uvunaji halali.
TARATIBU ZA UVUNAJI NA USAFIRISHAJI
Mhifadhi Mlela ameeleza kuwa ili kuvuna mkaa kutoka katika misitu ya asili kuna taratibu zakufuata, mtu anapaswa kuwasilisha maombi kwa Kamati ya Uvunaji inayoongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Mkuu wa Wilaya, Mhifadhi wa TFS akiwa Katibu na viongozi wa vijiji husika yaani watendaji na wenyeviti, baada ya uthibitisho wa umiliki wa shamba, amesema leseni hutolewa kwa ajili ya mavuno kama mkaa, kuni au mbao.
“Baada ya leseni kutolewa, mhusika hupaswa kuchukua hati ya usafirishaji, akieleza aina ya chombo atakachotumia pamoja na mahali mkaa unapopelekwa, lengo ni kuweka ufuatiliaji thabiti,” alisema Mlela.
MALALAMIKO KUTOKA KWA WANANCHI
Licha ya ufafanuzi huo, wananchi wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa bei ya mkaa na ugumu wa upatikanaji wake, Edward Kamilo kutoka Mkuzo Manispaa ya Songea, amesema bei ya mkaa imepanda hadi kulazimika kutumia mabunzi ya mahindi ambayo huuzwa kwa Shilingi 7,000 kwa ndoo ndogo.
“Tunaiomba Serikali iangalie upya sheria hii hasa kwa kuzingatia kundi la mama ntilie ambao wanategemea mkaa kwa shughuli zao za kila siku, wengi wanahangaika kupata mkaa wa kupikia,” alisema Kamilo.
Katika eneo la Lizaboni kwa Bibi 26 mwananchi mmoja alieleza kuwa ameshindwa kupika maharage kwa sasa kutokana na mkaa kupanda bei, huku bei ya chakula cha mama ntilie ikipanda hadi Sh 2,500 kwa sahani. Wengine wameshauri Serikali kufikiria kuruhusu matumizi ya makaa ya mawe kama mbadala wakati huu wa uhaba.
Jovine aliongeza kuwa ni vigumu kwa mtu wa kipato cha chini kumudu gharama za usafiri wa gunia moja la mkaa kupitia gari, akiiomba Serikali iangalie upya sheria hiyo kwa jicho la huruma kwa wananchi wa kawaida.
HALI YA UVUNAJI YAONEKANA KUONGEZEKA
Pamoja na changamoto hizo, TFS imesema kuwa hali ya uvunaji wa mkaa haijapungua bali inaendelea kuongezeka, tangu tarehe 1 hadi 24 Julai, leseni 308 za uvunaji wa mkaa zimetolewa.
Hata hivyo, Meneja Mlela amesema bado kuna tatizo katika mlolongo wa mnyororo wa usambazaji wa mkaa, hasa kutoka kwa wasambazaji hadi kwa watumiaji wa mwisho, alibainisha kuwa baadhi ya wasafirishaji wamekuwa wakipandisha bei kiholela, na TFS iko mbioni kufanya utafiti ili kujua kiini cha ongezeko hilo la bei.
“Hatujapandisha bei ya mkaa wala gharama za kupata leseni. Tunachokifanya sasa ni kujua kwa nini bei inakuwa juu sokoni, Tutakaa na Mkuu wa Wilaya tukutane na wafanyabiashara kutafuta suluhisho, na ikiwezekana kuwe na bei elekezi ya mkaa,” alisema Mlela.
Mabadiliko haya ya utaratibu wa usafirishaji wa mkaa yamekuja kwa nia njema ya kulinda mazingira na rasilimali za misitu, lakini yameibua changamoto kwa wananchi wa kawaida, hasa kwa wale wa kipato cha chini wanaotegemea mkaa kwa matumizi ya kila siku.
Ni wazi kuwa mafanikio ya sera hii yatategemea jinsi mamlaka zitakavyoshirikiana na wadau mbalimbali kuleta uwiano kati ya ulinzi wa mazingira, wananchi wametakiwa kuwa wavumilivu wakati mchakato wa ufuatiliaji wa malalamiko yao ukiwa unaendelea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...