Maonesho ya sanaa na mavazi ya utamaduni wa Kiswahili yaliyooneshwa jijini Stockholm tarehe 5 Julai, 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani.
Mgeni rasmi, Waziri wa zamani wa Masuala ya Usawa wa Jinsia wa Sweden, Mhe. Nyamko Sabuni, akihutubia kwa lugha ya Kiswahili katika maadhimisho hayo.
Mhe. Balozi Mobhare Matinyi, akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, jijini Stockholm, tarehe 5 Julai, 2025.

UMOJA wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden ukishirikiana na jumuiya za Watanzania waishio nchini humo, umeandaa na kufanikisha sherehe za maadhimisho makubwa ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika tarehe 5 Julai, 2025, jijini Stockholm.

Maadhimisho haya hufanyika duniani tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuanzia mwaka 2022 kufuatia azimio lililopitishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema kuwa Serikali imeazimia kukieneza na kukienzi Kiswahili duniani kote huku akielezea namna kilivyosambaa na kuongeza kuwa kwa ushawishi wa Tanzania, Kiswahili sasa ni lugha ya kikazi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri wa zamani wa Usawa na Jinsia nchini Sweden, Mhe. Nyamko Sabuni, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lakini aliyezaliwa Burundi na kukulia Tanzania kabla ya kuhamia Sweden. Mhe. Nyamko akitoa hotuba yake kwa Kiswahili alielezea namna kinavyoziunganisha nchi hizi akisema hata anapokuwa nchini Kenya kibiashara hutumia pia lugha ya Kiswahili.

Sherehe hizo zilifana kwa wingi wa vyakula na vitu mbalimbali vinavyoitangaza Tanzania na utamaduni wa Mswahili kama viungo, maonesho ya mitindo ya mavazi, sanaa za mapambo, ngoma, nyimbo, mashairi na hadithi za watoto.

Shughuli hii ya kipekee iliwakutanisha zaidi ya watu 500 ambao mbali ya Watanzania wengine walikuwa ni raia au wenye asili za nchi za Afrika Mashariki na Kati, Waswidi marafiki wa Tanzania na Mabalozi na wawakilishi wa nchi za Botswana, China, Eritrea, India, Japan, Kenya, Misri, Nigeria, Rwanda na Zimbabwe.

Wadhamini walioshirikiana na Ubalozi ni benki mbili za nchini, NMB na CRDB; Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kenzan Travel, Green Tours Tanzania na Monty's Glow.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...