WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili nchini Belarus na ametumia ziara hiyo kuwaalika wenye viwanda, makampuni na wafanyabiashara waje kuwekeza nchini.

Waziri Mkuu aliwaeleza wakuu wa taasisi aliokutana nao baadhi ya maeneo ya kimkakati kwenye uwekezaji ambayo ni elimu ya juu, afya, kilimo, TEHAMA, uendelezaji viwanda, madini na kukuza utalii. Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukuza uchumi wa Tanzania kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Kwa kuzingatia azma ya Rais Samia, Waziri Mkuu amewahakikishia wenye viwanda na wamiliki wa kampuni zinazotaka kuwekeza nchini, utayari wa Serikali ya Tanzania kushirikiana nazo kwa kuzipatia misaada stahiki zitakapokuja kuwekeza nchini. Amewasihi wenye viwanda vya matreka na mitambo ya kilimo wafungue matawi nchini Tanzania ikiwemo na vituo vya kuhudumuia matrekta (mechanization centres) ili huduma za matrekta ziweze kuwa karibu na wakulima.

Vilevile, jana jioni (Jumatano, Julai 23, 2025) Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo inayotumika kuchimba madini na magari ya migodini; na pia alitembelea kiwanda cha kutengeneza vifaa vya uokoaji na kuzima moto na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na viwanda hivyo ili kuondoa tatizo la uhaba wa vifaa hivyo nchini.

Kampuni na taasisi alizotembelea Waziri Mkuu ni pamoja na kampuni ya kuzalisha na kusambaza dawa na vifaa tiba ya Belmedepreparaty (Republican Unitary Production Enterprises); Kiwanda cha kuzalisha matrekta na mitambo ya kilimo (Minsk Tractor Plant – OJSC); Chuo Kikuu cha Kilimo cha Belarus (BSATU), Kiwanda cha kuzalisha na kusambaza vifaa vya kielektoniki (BelOMO); kiwanda cha uzalishaji na usambazaji wa mitambo na magari makubwa ya kwenye migodi (BELAZ JSC) na kampuni ya kutengeneza na kusambaza vifaa vya uokoaji na zimamoto (POZHSNAB LLC).

Aidha, katika ziara hiyo Waziri Mkuu Majaliwa alikutana na mwenyeji wake, Bw. Alexander Turchin ambapo kwa pamoja walishuhudia utiaji saini wa hati tatu za makubaliano zilizohusu mashauriano ya kisiasa na makubaliano ya kuendeleza sekta za kilimo na elimu.

Vilevile, walishuhudia utiaji saini wa mkataba baina ya Chama cha Wafabiashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania (TCCIA) na Chama cha Wafabiashara wa Belarus unaolenga kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Waziri Mkuu Majaliwa pia alikutana na Wawakilishi wa Muungano wa Kampuni za Belarus zinazofanya biashara na mataifa ya Afrika (AFTRADE); na aliweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya mashujaa.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Bw. Shariff Ali Sharriff, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Dkt. Stephen Nindi na Balozi wa Tanzania nchini Urusi na Belarus, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...