Na Diana Byera,Bukoba.

Wakandarasi walioshinda dhabuni ya kutekeleza Miradi ya TACTICS Manispaa ya Bukoba yenye thamani ya shilingi bilioni 40 wamekabidhiwa maeneo ya kutekeleza miradi tarajiwa kutekelezwa katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Akiongea na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa alisema kuwa wakandarasi wamekabidhiwa maeneo ya ujenzi wa Soko Jipya la Manispaa ya Bukoba, Stendi ya Mabasi Kyakailabwa, ujenzi wa kingo za Mto Kanoni zenye urefu wa kilometa 7.3 pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara kilometa 10.75 ukiambatana na usimikaji wa taa za barabarani 423.

Alisema kuwa miradi hiyo imegawanywa katika makundi mawili ambapo Mkandarasi mzawa M/s Dimetoclasa Realhope Limited atajenga soko na Stendi ya Mabasi Kyakailabwa kwa gharama ya shilingi bilioni 18.9.

Aidha, Mkandarasi wa kigeni M/s Shandon Luqiao Group Company Limited atajenga barabara kilometa 10.75, kingo za Mto Kanoni kilometa 7.3 na kuweka taa za barabarani 423 kwa gharama ya shilingi bilioni 21.3.

Alisema kuwa matarajio yake ni kuona miradi hiyo inakamilishwa kwa wakati kulingana na mkataba ambapo wamepewa kipindi cha miezi 15 kuanzia Julai 15, 2025 hadi Oktoba 14, 2026.

"Miradi hiyo inatarajia kusisimua Manispaa ya Bukoba na mkoa wa Kagera kwa ujumla kwa kutengeneza maelfu ya ajira kwa vijana lakini pia kuwa kivutio kwa wananchi, hivyo nawataka wananchi kuhakikisha wanailinda miradi hiyo na kuwapa ushirikiano wakandarasi kufanya kazi yao bila vikwazo vyovyote."

Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Stephen Byabato aliishukuru serikali kwa kuridhia kutekeleza miradi hiyo. Ameishukuru serikali kwa kuridhia kutoa fedha za kutekeleza miradi hiyo.

Alisema kuwa kimekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi kuomba stendi mpya huku viongozi wengi waliopita wakishindwa kutegua kitendawili hicho.

Alisema moja ya ahadi za Chama Cha Mapinduzi katika kutafuta kura za mwaka 2020 ilikuwa ni ahadi kwa wananchi kuwa watapata soko la kisasa na stendi ya kisasa.

Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji 15 ya awamu nyingine zinazotekeleza miradi ya TACTICS, lengo likiwa ni kupendezesha miji na kuongeza mapato ya ndani.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...