SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wote wanaofanya shughuli kupitia majukwaa ya kidigitali kama Airbnb, Booking.com, Meta (Facebook, Instagram) na mingineyo, kujisajili rasmi na kuanza kuchangia kodi, la sivyo watakumbana na hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Yusuph Mwenda, amesema hayo leo Julai 24, 2025 wakati wa Uzinduzi wa uzinduzi wa utekelezaji wa makubaliano kati ya TRA na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya Kodi (IBDF)
Amesema "Nchi yetu imefungua milango ya uwekezaji duniani sasa tunayo makampuni ya kimataifa yanayolipa kodi na mengine yanakwepa hasa wale wa biashara za mtandaoni (digital platforms) kama Airbnb.
“Tuna makampuni mengi ya kimataifa yanayofanya biashara nchini, baadhi hulipa kodi lakini yapo ambayo hukwepa. Mafunzo haya kwa watumishi wetu yanalenga kuwajengea uwezo wa kubaini mianya hiyo, hasa kwenye eneo la uchumi wa kidigitali,” amesema Mwenda.
Kwa mujibu wa TRA, makampuni ya kidigitali hutoa huduma zinazowawezesha watu wengine kufanya biashara kwa urahisi, lakini yameleta changamoto kubwa ya usimamizi wa kodi kutokana na baadhi ya watumiaji wake kutokujisajili wala kutoa risiti.
“Kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 30, wale wote wanaopangisha nyumba kupitia Airbnb na majukwaa mengine, au wanaouza bidhaa mtandaoni bila kusajiliwa TRA, wanatakiwa kujisajili. Muda huu ni wa neema – hawatatozwa penati, lakini baada ya hapo tutaanza kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria,” aliongeza.
Aidha TRA imetangaza kuanzisha kampeni maalum nchi nzima, Bara na Visiwani, ya kuwaelimisha wafanyabiashara wa kidigitali juu ya umuhimu wa kujisajili, kupata namba ya mlipa kodi (TIN), na kutumia mfumo wa kutoa risiti kwa njia ya kielektroniki (EFD).
“Tumeweka mazingira rafiki. Tuna App ya EFD ambayo mtu anaweza kutumia kutoa risiti moja kwa moja kutoka kwenye simu, hata bila kuwa na mashine ya gharama kubwa. Tutaelimisha wananchi nchi nzima kuhusu hili,” alisema.
Aidha, Mwenda alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za watu wanaofanya biashara bila kulipa kodi ili kusaidia taifa kukusanya mapato sahihi na kulinda ushindani wa haki kwa wafanyabiashara wote.
“Tunao maofisa wetu walioko katika kila mkoa wanaofuatilia shughuli hizi. Lakini pia mitandao yenyewe inashirikiana nasi kupitia mifumo ya malipo ya Benki Kuu na TCRA Hivyo tukipata taarifa, tuna uwezo wa kuwafuatilia.”
Kampeni hiyo imekwenda sambamba na mafuzo kwa watumishi wa TRA kuhusu usimamizi wa kodi za kimataifa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa nchi kuhimili kasi ya mabadiliko ya kiuchumi duniani na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya ndani ambapo jumla yabwahitimu 18 wametunukiwa vyeti
CPA Mwenda amesema wapo wanafanya biashara wa mtandaoni ambao mizigo yao ipo nyumbani nao pia wanatakiwa kulipa kodi iwapo kipato chao kinafika sh. 4,000,000 kwa mwaka.
Amesema ofisi yake inayo mifumo ya kuwabaini wafanyabiashara wote hivyo amewataka wajisajili kwa hiyari na kupewa namna bora ya kutoa risiti kidijitali baada ya mauzo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Profesa Isaya Jairo amesema ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa kitaalamu wa watumishi wa TRA katika nyanja za kimataifa za kodi, hususan wakati ambapo taifa linaelekea kutimiza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
“Tunapozindua utekelezaji wa MoU hii, tunaweka msingi imara wa mafunzo endelevu, tafiti za pamoja, makongamano ya kimataifa, na maendeleo ya wataalamu wetu kupitia fursa za masomo na kubadilishana uzoefu,” amesema Prof. Jairo.
Naye, Profesa Victor van Kommer, kutoka IBDF amesisitiza umuhimu wa kuendeleza majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi, kutoa elimu endelevu, na kujenga mazingira bora ya biashara. Aliongeza kuwa kuongeza wigo wa kodi nchini kutasaidia serikali kuwekeza katika sekta muhimu kama elimu, afya, na miundombinu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...