
Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda na Mkurugenzi Mkazi wa Enabel nchini Tanzania, Koenraad Goekint wakibadilishana hati za Makubaliano ya Ushirikiano kwa lengo la kuimarisha ubora katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) yatolewayo nchini.

.jpeg)
Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABEL) zimesaini Makubaliano ya Ushirikiano kwa lengo la kuimarisha ubora katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) itolewayo nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda na Mkurugenzi Mkazi wa Enabel nchini Tanzania, Bw. Koenraad Goekin, leo tarehe 16 Julai, 2025 katika ofisi za NACTVET, Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam.
Dkt. Lingwanda, amebainisha kuwa makubaliano hayo yamejikita zaidi katika kuvijengea uwezo vyuo vya TVET nchini vibobee katika masuala ya uthibiti ubora na kuwa na uwezo wa kutoa mafunzo bora, kuimarisha miundombinu ya kujifunzia na ujifunzaji, na kukuza viwango vya ubora wa walimu ili kuzalisha wahitimu wanaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Mkurugenzi Mkazi wa Enabel nchini Tanzania, Bw. Koenraad Goekint, amesema ushirikiano kati ya ENABEL na NACTVET utasaidia katika kuhakikisha mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya TVET yanaendana na viwango vinavyokubalika na vyenye kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Bw. Goekint amesema makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa “Wezesha Binti” unaotekelezwa nchini kwa lengo la kuwapatia ulinzi na usawa kwa kijinsia vijana wa kike kwa kuwapatia elimu na ujuzi ili kuwaongezea fursa za ajira.
Aidha, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora NACTVET, Dkt. Jofrey Oleke, amesema utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza kwa kufanyika tathmini ya hali ya uthibiti ubora katika vyuo vya TVET nchini na kuandaliwa Mwongozo wa Udhibiti Ubora utakaowezesha kuongezeka kwa ubora kwenye vyuo vya TVET.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...