WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selamani Jafo, amesema kuwa ndani ya muda mfupi Tanzania haitahitaji tena kuagiza bidhaa muhimu kama mabati, vioo, nondo na saruji kutoka nje ya nchi, kutokana na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Jafo tarehe 31 Julai 2025 wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkoa wa Pwani, ambapo alizindua rasmi Kongani ya Viwanda ya Kwala pamoja na Bandari Kavu ya Kwala.

“Kwa mfano, mahitaji ya mabati kwa mwaka ni tani 130,000. Leo hii, makampuni yote yanayozalisha mabati hapa nchini, ikiwemo Lodhia, King Lion, Alaf na mengineyo, yamefikia uzalishaji wa tani 260,000 kwa mwaka. Hii ina maana tunakuwa na ziada ya tani 130,000,” alisema Waziri Jafo.

Aliongeza kuwa hatua hii ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kuwa Tanzania inajenga uchumi wa viwanda unaojitosheleza kwa bidhaa za msingi, huku pia ikiongeza uwezo wa kusafirisha bidhaa nje ya nchi na kuingiza fedha za kigeni.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, Eneo la Kwala lina zaidi ya hekta 1,000, ambapo zaidi ya viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa kwa uwekezaji unaozidi dola za Kimarekani bilioni 3. Inakadiriwa kuwa bidhaa zitakazozalishwa kwenye kongani hiyo zitaweza kuingiza jumla ya dola bilioni 6 kwa mwaka, ambapo dola bilioni 4 zitabaki kwa matumizi ya ndani, na dola bilioni 2 zitatokana na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.

Waziri Jafo alisisitiza kuwa Wizara itaendelea kusimamia maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji wa bidhaa Afrika Mashariki, na sehemu nyingine duniani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...