*Profesa Mkenda amshukuru Rais Dkt. Samia kwa maboresho katika sekta ya elimu
*Waajiri wanaowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati wapewa Tuzo
*Waajiri wavutiwa na maboresho ya huduma za kidijiti
Na MWANDISHI WETU, Mwanza
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetoa elimu ya hifadhi ya jamii na kueleza maboresho mbalimbali ya huduma zake, katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake Wamiliki wa Shule na Vyuo vya Kati Tanzania (TAWOSCO), uliofanyika tarehe 23 Julai, 2025 jijini Mwanza.
Akifungua mkutano huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolf Mkenda alieleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na TAWOSCO katika sekta ya elimu, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya kwenye sekta ya elimu nchini.
Katika hafla hiyo, Prof. Mkenda alikabidhi tuzo kwa waajiri wanaowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati katika Mfuko wa NSSF, ikiwa ni njia ya kutambua na kuthamini uadilifu wao katika kutekeleza wajibu huo muhimu wa kisheria na kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Saidi Mtanda aliwapongeza wanawake wa TAWOSCO kwa mchango wao kwenye maendeleo ya elimu, sambamba na kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwekeza katika mkoa huo, hususan kuboresha miundombinu ya elimu na huduma za kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja wa Uandikishaji, Ukaguzi na Matekelezo wa Mfuko huo, Bw. Cosmas Sasi alieleza kuwa hadi sasa, wanachama 131 wa TAWOSCO sawa na asilimia 66 wamejiunga na NSSF, huku wanachama 35 kati yao wakichangia michango ya wafanyakazi wao kwa ufanisi kila mwezi.
Aidha, Bw. Sasi aliwasihi wanachama wenye malimbikizo ya michango kufika katika ofisi za NSSF ili kuwasilisha mipango ya ulipaji wa madeni yao, badala ya kusubiri hatua za kisheria ambazo zinaweza kuepukika kwa kushirikiana kwa karibu na Mfuko.
Akizungumzia maboresho ya huduma, Bw. Sasi alisema kuwa Mfuko umeanzisha mifumo ya kidijitali kama vile NSSF Portal yaani Lango la Huduma linalojumuisha huduma binafsi ya mwanachama, huduma binafsi ya mwajiri, NSSF App, WhatsApp Chatbot, huduma za USSD na SMS, ambazo zinawezesha wanachama na waajiri kupata huduma kwa urahisi zaidi bila kulazimika kufika ofisini.
Katika risala yao, Makamu Mwenyekiti wa TAWOSCO, Bi. Christa Rweyemamu alieleza kuwa Umoja huo unajumuisha wanachama 195 wanaohudumia wanafunzi 900,000 na kuajiri zaidi ya watu 5,000. Alitoa shukrani kwa NSSF na wadhamini wengine kwa kushiriki na kutoa elimu muhimu katika mkutano huo.
Baadhi ya washiriki walieleza kufurahishwa na maboresho ya huduma za TEHAMA zinazotolewa na NSSF, wakisema kuwa zimewawezesha kupata huduma nyingi kwa haraka na kwa urahisi kupitia simu zao za kiganjani, hali inayowawezesha kuokoa muda na gharama za usafiri.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...