Na. Elimu ya Afya.

SERIKALI imetoa wito kwa jamii kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu kwa kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kutumia maji safi na salama pamoja na vyoo bora.

Hayo yamebainishwa leo Julai 9, 2025 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Epidemiojia na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vida Mmbaga akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali katika Kikao Kazi cha Kuhakiki Maeneo hatarishi kupata ugonjwa wa Kipindupindu (PAMI’s) kilichoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani(WHO)

Dkt. Mmbaga amesema ni muhimu kwa kila mtu na jamii kwa ujumla kuzingatia kanuni za usafi hasa umuhimu wa matumizi ya maji safi na salama na matumizi sahihi ya vidonge vya kutibu maji pamoja na matumizi sahihi ya vyoo bora.

“Ugonjwa wa Kipindupindu unasababishwa na kinyesi kibichi cha binadamu ambacho kinaweza kuingia kwenye maji , hivyo sisi kama Serikali kupitia kikao hiki cha kuhakiki kitasaidia kuweka mikakati ya pamoja katika kuzuia kipindupindu sehemu ambazo zimekuwa zikikumbwa na kipindupindu mara kwa mara, ” amesema.

Aidha, Dkt. Mmbaga amesema Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vidonge vya kutibu maji vinapatikana huku akizungumzia mkakati wa kidunia wa kumaliza Kipindupindu ifikapo mwaka 2030.

“Serikali imekuwa na mkakati wa kuhakikisha kipindupindu kinatokomezwa kwa zaidi ya asilimia 90 ifikapo mwaka 2030, hivyo kikao hiki ni muhimu sana kubaini maeneo yanayokumbwa na kipindupindu na kuweka mikakati ya pamoja katika kudhibiti ugonjwa huo ”amesema Dkt. Mmbaga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Masuala ya Dharura kutoka Shirika la Afya Duniani Ukanda wa Afrika (WHO-Afro) Dkt. Dick Chamla ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na WHO katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu ambapo pia amesema Shirika la Afya Duniani lilianzisha mkakati kabambe wa kupambana na kipindupindu .

“WHO ukanda wa Afrika imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ugonjwa wa kipindupindu ambapo pia Serikali ilichukua hatua madhubuti na ninashukuru kwa Tanzania kwa kuwa imara katika kupambana na magonjwa ya mlipuko, hivyo kupitia kikao hiki kutakuwa na mchango mkubwa wa kuainisha maeneo yanayokumbwa na kipindupindu na kuchukua hatua satahiki katika kupambana na ugonjwa huo”amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...