Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164 na kibali cha uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa.

Taarifa ya Tume kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Julai 19,2025 na kusainiwa na mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ndg. Ramadhani Kailima imesema Tume imefikia uamuzi wa kutoa vibali hivyo katika kikao chake kilichokutana Julai 18, mwaka huu.

“Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 10(1) (g) (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 22 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, katika kikao chake maalum kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 Tume imeridhia na kutoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164.,”alisema taarifa hiyo ya Tume.

Aidha, Kailima amesema katika kikao hicho imeridhia na kutoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa.

Taarifa hiyo ya Kailima imesema Tume imefanya uamuzi huo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 10(1)(i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024 kikisomwa pamoja na kifungu cha 85(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024 na kanuni ya 13(1) na (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.

Orodha ya taasisi na asasi husika inapatikana kupitia tovuti ya Tume ya www.inec.go.tz na mitandao ya kijamii ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

“Taasisi na asasi za kiraia zilizoridhiwa na kupewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura zitajulishwa kwa njia ya barua pepe kupitia Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System) ili kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu nyingine ikiwemo kuweka orodha ya watu watakaotoa elimu hiyo,”imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Tume.

Aidha, Kwa upande wa taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi zimetakiwa kuwasilisha kwa njia ya Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System) majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uangalizi huo kwa ajili ya kuwaandalia vibali.

Tume imebainisha kuwa, taarifa zingine zote muhimu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa elimu ya mpiga kura na uangalizi wa uchaguzi, miongozo na taratibu zote zitatolewa mapema iwezekanavyo.

Tume imezipongeza taasisi na asasi za kiraia ambazo zimepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na kuwa waangalizi wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...