TUZO ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika imetangaza washindi wa miswada ya mashindano ya mwaka 2024 katika hafla ya kufana iliyofanyika katika Chuo Kikuu Dar es Salaam huku watanzania wakiibuka kidedea katika mashindano hayo ya tisa tangu kuanzishwa kwake 2015.

Tuzo hii, iliyoanzishwa na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma Wa Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha hizo, baina ya lugha hizo na kwa lugha hizo, inafadhiliwa na kampuni ya Safal Group, kupitia ALAF-Tanzania na Mabati Rolling Mills-Kenya.

Mshindi wa kwanza katika kipengele cha Riwaya ni Mayasa Abdalla (Mtanzania) aliyejinyakulia kitita cha $5000 kwa kuwasilisha mswada ujulikanao kama ‘Kitanzi cha Mauti.

Mshindi wa pili katika kipengele hicho ni Ali Othman Masoud (Mtanzania) aliyewasilisha mswada ujulikanao kama ‘Nyaraka za Wafu’ huku akipata $2500 kama zawadi.

Katika kipengele cha Ushairi, mshindi ni Bashiru Abdalla (Mtanzania) mwenye mswada ujulikanao kama ‘Bure Ghali’ambaye alipata zawadi ya $5000 huku Mohamed Idrisa (Mtanzania) akishika nafasi ya pili kupitia mswada wake-‘Laana ya Uovu’ uliomzolea $2500.

Mshiriki kutoka Kenya, Edwin Omindu alitangazwa mshindi wa kipengele cha Hadithi Fupi kupitia mswada wake – ‘Mungu Hadanganywi’ huku akizawadiwa kitita cha $2500.

Waziri wa Utamaduni, Habari, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi alitoa pongezi kwa washindi wote kwa kazi nzuri na kuipa kongole Safal Group kwa kuwa mstari wa mbele katika kukienzi Kiswahili mwaka hadi mwaka.

“Mashindano haya yamekuwa maarufu na kuzidi kuvutia washiriki wengi wakiwemo baadhi kutoka katika mabara mengine kutokana na umuhimu wa lugha hii ya Kiswahili ambayo ni tunu yetu kwa hivyo lazima tujivunie na tukienzi ipasavyo,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza lugha ya Kiswahli kwani inatumika katika nchi nyingi za Kiafrika na baadhi ya nchi za ulaya wanakifundisha vyuoni ambayo ni fursa nzuri ya ajira kwa Watanzania.

Alipongeza pia Mkuki na Nyota Publishers na Africa Poetry Book Fund ambao ni wachapishaji wa miswada iliyoshinda, huku akitoa wito kwa mashirika mengine yajitokeze kuunga mkono jitihada hizi za kukienzi Kiswahili.

Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Tanzania, Ashish Mistry alisema kampuni ya Safal Group ambayo ni kampuni mama ya ALAF Tanznaia na Mabati Rolling Mills ya Kenya, imeendelea kudhamini tuzo hizo kutokana na ukuajia wake mwaka hadi mwaka na umuhimu wa Kiswahili katika kuunganisha bara la Afrika.

Mwenyekiti wa majaji wa mashindano ya mwaka 2024, Dkt Salma Hamad, wa Chuo Kikuu Huria, Tanzania, alisema “Miswada ilikuwa mingi hata hivyo tumeburudika vya kutosha kwa sababu tumesoma kazi zilizoandikwa na kusukwa kiubunifu na tumejifunza kwamba kuna hazina kubwa ya vipaji vya uandishi wa fasihi ya kiswahili. Vikiendelezwa fasihi ya Kiswahili haitafilisika.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo hii, Abdilatif Abdalla, aliongeza, “Ni jambo la kufurahisha mno kuona kwamba tangu mashindano yalipoanzishwa mwaka 2015, bado Tuzo hii inaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa. Pia kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka, na kwa hivyo kuitajirisha Fasihi ya Kiswahili.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...