
WASHIRIKI zaidi ya 2000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki kongamano la mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) linalotarajiwa kufanyika Agosti 11 hadi 13 mwaka huu mkoani Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 4, 2025, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala amesema wanategemea washiriki hao wataungana nao katika tukio hilo muhimu kwa musktakabali wa sekta ya NGOs na taifa kwa ujumla.
Amesema kongamano hilo limeandaliwa kwa pamoja kati ya NaCoNGO na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Ofisi ya Msajili wa NGOs huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.
“Kaulimbiu ya kongamano hili ni ‘Tathmini ya miaka mitano ya mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya taifa, mafanikio, changamoto, fursa na matarajio’, tunaamini mashiriki yote yaliyopo nchini yatajitokeza kwa wingi kushiriki,” amesema
Aidha amesema kama sehemu ya maandalizi ya kongamano hilo kumekuwa na majukwaa ya mashirika yasiyo ya kiserikali ngazi za wilaya na mikoa ambayo yamefanyika na mengine yanaendelea kufanyika.
“Wageni rasmi kwenye majukwaa ngazi za wilaya na mikoa ni wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, natumia nafasi hii kuwashukuru wakuu wa wilaya zote 103 na wakuu wa mikoa 14 ambao wamefanikisha majukwaa katika ngazi zao.
“Tunawaalika viongozi, wanachama na wanufaika wa mashirika yote yasiyo ya kiserikali, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na wadau wote kujisajili kushiriki katika kongamano kwa njia ya mtandao huu https://s.zoom.us/m/bPFinJyC0,” amesema
Naye Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara, Vickness Mayao amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuhakikisha mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali umekuwa ukithaminiwa.
Amesema majukwaa hayo katika shughuli zao wamekuwa wakipata wageni rasmi ambao ni wakuu wa nchi na kwamba hiyo inaonesha wazi dhamira ya serikali katika kushirikiana na mashirika hayo katika nyanja zote.
“Kila mwaka tumekuwa tukitathmini mchango wa mashirika haya na kwa upanda zaidi mwaka huu tumesema tutaangalia mchango wao kwa miaka mitano, tutaangalia maeneo mbalimbali ya tathmini ikiwemo mafanikio yao,” amesema
Aidha amesema anawakaribisha wadau wote kushiriki katika kongamano hilo ambao linawaleta pamoja mashirika hayo ambayo yamekuwa yakichagiza kazi mbalimbali za maendeleo nchini.
Kwa upande wake Meneja Kitengo cha Mashirika yasiyo ya Kiserikali Benki ya Stanbic, Naomi Vicent amesema benki hiyo inaendelea kushirikiana NGOs kwa kuwapatia huduma bora za kifedha na hatimaye wawahudumie wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...