Kutokana na fursa zinazotolewa kwa wananchi kupitia Programu ya Imbeju, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ameipongeza Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kukuza ujasiriamali na kuongeza elimu ya fedha kwa wananchi wengi zaidi.
Waziri Kikwete ametoa pongezi hizo kwenye uzinduzi wa shirika lisilo la kiserikali linalohamasisha ujasiriamali miongoni mwa vijana la National Enterprise Development Chamber (NEDC) uliofanyika mwishoni mwa wiki.
“Taasisi ya CRDB Bank Foudation mnafanya kazi kubwa sana katika kuwainua vijana kupitia Programu yenu ya Imbeju. Mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha mnayoitoa. Kujitoa kwenu kuilea NEDC nalo ni jambo muhimu litakalosaidia kuwajumuisha vijana wengi kwenye huduma rasmi za fedha,” amesema Waziri Kikwete.
CRDB Bank Foundation imedhamini uzinduzi wa NEDC inayoziunganisha biashara changa hasa za kibunifu ambazo nyingi zinamilikiwa na vijana, kuwaunganisha wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na taasisi za umma ili kujenga ushirikiano utakaoboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, malengo ambayo ni miongoni mwa vipaumbele tunavyotekeleza CRDB Bank Foundation.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema wanashirikiana na kila mdau kuboresha maisha ya watu kutoka jamii zilizotengwa kifedha na kiuchumi kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya fedha na kuwapa mitaji wezeshi wajasiriamali wanaokidhi vigezo.
“Katika kuhamasisha maendeleo ya ujasiriamali na ubunifu, tunachochea ukuaji wa ubunifu na biashara changa za vijana, tunawawezesha vijana na wanawake kupitia mafunzo ya stadi za elimu ya fedha, ujasiriamali, usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu na mbinu za upatikanaji wa rasilimali fedha pamoja na Kuchochea ubunifu kupitia programu za kukuza na kuendeleza biashara changa,” amesema Tully.
Ili kuwa na maisha bora, Tully amesema ni muhimu kwa wananchi hasa wa kipato cha chini kujengewa wa kifedha , kukuza utamaduni wa kuweka akiba na uwekezaji pamoja na kuwajumuisha katika huduma rasmi za fedha vijana na wanawake bila masharti magumu.
“CRDB Bank Foundation (CBF) inatambua nguvu ya ushirikiano wa kimkakati katika kuleta mabadiliko chanya kwani ndio njia ya uhakika ya kufungua fursa zaidi kwa vijana na wanawake wajasiriamali nchini. Tunashirikiana na serikali kuendeleza ujumuishaji wa kifedha na kukuza suluhisho bunifu na tunashirikiana na sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika ujasiriamali na elimu ya fedha,” amesema Tully.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji tena National Enterprise Development Chamber (NEDC), Jesse Madauda amesema wataendelea kushirikiana na serikali, taasisi za umma na binafsi pamoja na wabia wengine wanaopenda kumwinua Mtanzania kiuchumi.
“Kwa kuunganisha nguvu, rasilimali na mikakati, tunaamini tunaweza kuharakisha ukuaji wa biashara changa zenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika jamii,” amesema Madauda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...