Na Seif Mangwangi, Arusha

MAAFISA usafirishaji wa abiria maarufu kama 'bodaboda', wametakiwa kukumbuka kuweka akiba kupitia mapato wanayoyapata na kujijenga zaidi kiuchumi badala ya kufanya anasa kwa kuhonga mapato hayo na mwisho kuporomoka kiuchumi.

Akifungua mafunzo ya ujasiriamali, Usalama barabarani, Afya na Mazingira kwa waendesha bodaboda jana Agosti 15,2025 jijini Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenan Kihongosi,amesema bodaboda wamekuwa wakipata fedha nyingi lakini kwa kukosa maarifa sahihi wamekuwa wakishindwa kuendelea.

Amesema mafanikio katika biashara yanahitaji mipango mizuri ya kifedha na kuwataka bodaboda kama wasafirishaji kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha wanatengeneza bajeti na kuziheshimu,

" Wekezeni akiba kwa ajili ya dharura au kuanzisha miradi mipya; tumia faida kukuza biashara badala ya matumizi ya anasa,". Amesema.

Mkude amesema afya njema ni mtaji wa kwanza wa mjasiliamali na kuwataka bodaboda kujiunga na utaratibu wa kupata bima ya afya na endapo watakwama atakuwa tayari kuwasaidia.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya elimu ya Watu Wazima nchini (TEWW), Profesa Philipo Sanga amesema Wilaya za Longido na Monduli Mkoani Arusha zinaongoza kwa kuwa na watu wazima wasiojua Kusoma, Kuhesabu na Kuandika

Amesema miongoni mwa kundi hilo wapo maafisa usafirishaji maarufu bodaboda na hivyo kuuomba uongozi wa Mkoa wa Arusha kuangazia wilaya hizo ili kutokomeza tatizo hilo.

Profesa Sanga amesema kwa mujibu wa sensa na watu na makazi ga 2022 takribani asilimia 17 ya watanzania hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu huku Arusha pekee ikiwa na jumla ya watu asilimia 15.2 wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika.

Amesema kukosa stadi hizo ni changamoto inayoathiri uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

" Stadi za kusoma,Kuandika na Kuhesabu (KKK), ni msingi wa maendeleo, ni vigumu kuendesha biashara kwa ufanisi, kusoma alama za usalama barabarani, kuhesabu mapato na matumizi na kupata fursa za mikopo ambayo mara nyingi huhitaji ujaze nyaraka muhimu," amesema.

Amesema katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo, taasisi ya elimu ya watu wazima kwa kushirikiana na ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga kusaidia wale wote wasio na stadi za KKK ili kuwaondoa katika wimbi la ujinga.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...