Na Mwandishi wetu Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhe. Athumani Kilundumya, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuimarisha ushirikiano na sekta ya kilimo katika kuleta mapinduzi ya kidijitali katika sekta hiyo.

Mhe. Kilundumya ameyasema hayo wakati alipotembelea banda la e-GA katika maonesho ya Kilimo na Wafugaji “Nanenane” yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Alibainisha kuwa, Wizara ya Kilimo imeshuhudia jitihada mbalimbali zinazofanywa na e-GA katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya sekta ya kilimo ili kuimarisha sekta hiyo.

“Natambua jitihada za e-GA ikiwemo ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa mbolea kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) ambao unawezesha usajili na utoaji wa leseni  kwa wauzaji na wasambazaji wa mbolea, utambuzi wa maghala ya utunzaji wa mbolea pamoja na udhibiti wa soko la mbolea” alifafanua.

Aliongeza kuwa, kupitia mfumo huo Serikali inaweza kudhibiti soko la mbolea na kuhakikisha mbolea inauzwa kwa bei rafiki kutokana na ruzuku ya Serikali katika mbolea na hivyo wakulima kuweza kulima na kupata faida.

Aidha, alitaja taasisi nyingine zilizoshirikiana na e-GA katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA kuwa ni pamoja na Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika kwa kujenga Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushiriki na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kujenga Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Umwagiliaji.

“Nafahamu kuna Mfumo wa eKilimo ambao unarahisisha utendaji kazi katika sekta ya kilimo natamani kuona baadaye mfumo huu ukituwezesha kupata taarifa za wakulima wote hata wale wadogo waliopo vijijini ambao hawajasajiliwa, ni Imani yangu Wizara tukileta mahitaji haya e-GA mtayafanyia kazi”, alifafanua.

Naye Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Bi. Subira Kaswaga, amemshukuru Naibu Waziri kwa kutembelea banda la e-GA na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa sambamba na kuendeleza ushirikiano wa e-GA na sekta ya kilimo katika kuimarisha TEHAMA katika taasisi hiyo.

Alisema kuwa, e-GA imekuwa mstari wa mbele katika kutengeneza bunifu za mifumo ya kimkakati kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi ya kidijitali kwa jamii ya mijini na vijijini.

Maonesho ya kitaifa ya nanenane ,mwaka 2025 yanafanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...