
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) Olesumayan Daniel akizungumza kuhusiana na mafanikio ya Bodi katika kipindi cha awamu ya Sita ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri akitoa maelezo kuhusiana na uratibu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo kuzungumzia maendeleo.
Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari katika mkutano wa GBT.
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
BODI ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imetangaza mafanikio makubwa ya kiuchumi katika Awamu ya Sita ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukusanya mapato yaliyofikia zaidi ya shilingi bilioni 260.21, ikilinganishwa na shilingi bilioni 131.99 zilizokusanywa awali.
Akizungumza katika kikao na wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa GBT, Bw. Olesumayan Daniel, alisema kuwa jumla ya shilingi bilioni 922.25 zimekusanywa kupitia kodi, huku ajira zaidi ya 30,000 zikizalishwa kupitia sekta hiyo.
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, GBT imetoa leseni ya Bahati Nasibu ya Taifa kwa kampuni ya Ithuba Tanzania Limited, inayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 40 na wawekezaji kutoka Afrika Kusini kwa asilimia 60. Kampuni hiyo imewekeza zaidi ya USD milioni 20 (sawa na shilingi bilioni 50) na imeanza rasmi shughuli zake mwezi Aprili 2025.
Bw. Daniel alisisitiza kuwa michezo ya kubahatisha ni burudani, siyo ajira, hivyo washiriki wanapaswa kucheza kwa nidhamu bila kuhatarisha maisha yao kifedha.
Aidha, alibainisha kuwa asilimia tano ya mapato ya bodi hutumika kuendeleza michezo nchini. Hadi sasa, kati ya shilingi bilioni 44 hadi 53 zimetolewa kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya michezo.
GBT pia imesajili kampuni 62 zenye michezo ya kubahatisha 8549, lakini changamoto kubwa imebaki kwa waendeshaji wasio na leseni. Hatua zimechukuliwa kuhakikisha watoto hawashiriki kabisa katika michezo hiyo.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kiasi cha shilingi bilioni 66.7 kimeingizwa nchini kutoka kwa wawekezaji wapya katika sekta hiyo, na uwekezaji zaidi unatarajiwa kuongezeka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...