Na Mwandishi Wetu, Kyela
ALIYEKUWA mtia nia wa kuteuliwa kugombea Ubunge wa Jimbo la Kyela kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Godlove Mwakibete maarufu kama Chief Godlove, amerejea kwa wananchi wa Kyela kuwashukuru kwa imani waliyoionesha kwake kabla ya jina lake kuondolewa na Kamati Kuu ya chama hicho katika mchakato wa uteuzi.
Godlove, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Chiefgodlove Foundation inayosaidia yatima, wajane na watu wasiojiweza, alikutana na wananchi wa jimbo hilo mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kutoa shukrani rasmi.
Katika hotuba yake, amesema pamoja na jina lake kutopenya katika hatua za mwisho za mchakato wa uteuzi, bado anaendelea kuwa na ndoto na dhamira ya kweli ya kuiletea maendeleo Kyela.
"Kukatwa kwa jina langu hakutazima ndoto zangu kwa Kyela. Nitazidi kushirikiana na marafiki zangu pamoja na wadau mbalimbali ili kuleta maendeleo. Lengo langu ni kuifanya Kyela kuwa mfano wa kuigwa nchini," alisema.
Godlove alisisitiza kuwa safari ya kisiasa ni ndefu na kuna wakati mafanikio yanachelewa kufika, lakini ni muhimu kutokata tamaa. Aliahidi kuwa atabaki kuwa bega kwa bega na wananchi wa Kyela na atatoa ushirikiano kwa mgombea atakayepitishwa.
"Naamini aliyepitishwa pia ana malengo mema kwa Kyela. Nitafanya kazi naye kwa ukaribu, kwa sababu maendeleo hayahitaji nafasi tu, yanahitaji moyo wa kweli," aliongeza.
Akitaja vipaumbele vyake, alisema moja ya ndoto zake kubwa ni kuwasaidia vijana na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya, ikiwemo bima ya afya kwa wote.
Aidha, alitoa shukrani kwa Chama Cha Mapinduzi na kuahidi kutoa ushirikiano kwa mgombea wa urais wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine wa chama.
"Nawaomba wana CCM wote tushikamane, tuwaunge mkono waliopitishwa na chama kwa sababu wao ndio wameaminiwa. Tugawane majukumu ya kuhakikisha chama kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao," alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walieleza namna walivyoguswa na hatua ya Godlove ya kurejea kuwashukuru na kuonyesha mshikamano licha ya kutopitishwa.
Atupile Mwakifulefule alisema:
"Tulikuwa na matumaini angepitishwa kwa sababu tulimwona anafaa. Lakini tunaheshimu maamuzi ya chama. Tunampongeza kwa kurudi kutushukuru."
Naye Charles Melkyori aliongeza:
"Chama kisiache kuwatumia vijana kama Godlove. Ameonyesha moyo wa dhati wa kusaidia jamii, si kwa kutafuta madaraka bali kwa upendo wa kweli."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...