Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
KATIBU Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Zena Ahmed Said ametoa wito ka washiriki 58 wanawake Viongozi wa Taasisi za umma na binafsi nchini kutokubweteka na vyeo ama nafasi zao za Uongozi katika sehemu zao za kazi bali wafanye kazi kwa wito na kuwa mfano wa kuigwa mahala pa kazi.
Amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya uongozi ya wiki moja kwa Wanawake Viongozi yanayofanyika kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwamfipa Kibaha , Mkaoni Pwani.
Zena amesema wakatumie vema mafunzo hayo katika kuongoza taasisi mbalimbali wanazoziongoza hapa nchini.
Na pia amewataka Wanawake hao Viongozi wasibweteke na majina ama vyeo vyao huku amewataka wawe na wito wa kujiendeleza wakati wote.
"Yachukulieni mafunzo haya kwa uzito wa hali ya juu , natoa pongezi kwa uongozi wa Shule ya Mwalimu Nyerere kwa uanzishwaji wa mafunzo haya kwani kiongozi bora ni yule ambaye amekua akijengewa uwezo mara kwa mara kwa sababu uongozi wa sasa siyo wa amri bali ni wa matendo zaidi" amesema Mhe. Zena.
Aidha Mhe. Zena amesema kuwa washiriki wote wanatakiwa kuwa na uthubutu katika kutafuta fursa mbalimbali bila woga .
"Natoa wito kwa Taasisi mbalimbali kuleta viongozi wao ili waweze kupata mafunzo ya uongozi kwani itawasaidia kuwajenga kiutendaji zaidi pia nimefurahia kuona mandhari ya hapa tulivu na mshiriki akiingia anazingatia masomo bila ya kupata changamoto ya aina yoyote" alisema Mh. Zena.
Wakati huo huo amesema kuwa wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais , Wabunge na Madiwani , amewataka akinamama hao kuwa chachu ya amani miongoni mwa watanzania wote ikiwa sambamba na kuchagua viongozi waadilifu kwa maslahi mapana ya nchi kwani ulinzi wa amani ya nchi iko mikononi mwa kila Mtanzania.
Awali alimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mazingira mazuri na rafiki kwa wanawake nchini kote na kuandika historia ndani na nje ya nchi yetu sambamba na kuongeza idadi ya Viongozi Wanawake nchini.
"Dkt. Samia amevunja vikwazo vya muda mrefu ambavyo vilikuwa vikiwakwamisha wanawake wengi kupata nafasi kubwa kwenye ngazi za uongozi lakini tangu alipoingia madarakani katika kipindi cha awamu ya sita" amesema Katibu Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Mh. Zena.
Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Prof. Marcelina Chijoriga amesema washiriki hao wa mafunzo watafundishwa uzalendo, itifaki, usalama wa taifa, umajumui na tunategemea mara watakapohitimu mafunzo yao watakuwa waminifu na waadilifu zaidi kwenye maeneo yao wanayoyaongoza hiyo ni baada ya kupfundishwa mbinu mbalimbali kutoka kwa wawasilishaji wabobevu.
Mkuu wa Shule ya Uongozi Profesa Marcelina Chijoriga amesema kuwa katika mafunzo hayo yanayoshirikisha washiriki kutoka katika Tasisi mbalimbali 19 za serikali huku washiriki wengine wanne wamejilipia wenyewe kutoka na utashi wa kujiendeleza akiwamo SSP Juliet Lyimo kutoka ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani amesema kuwa yeye amejilipia kutokana na lengo la kuamua kujijengea uwezo.
Mbali ya kuwa Shule inatoa mafunzo kwa Vyama na makada wa siasa pia Shule hiyo inatoa mafunzo kwa Taasisi binafsi na hata mtu mmojammoja ambao wanakua wanakidhi vigezo vya kupata huduma .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...