-STAMICO yafungua milango kwa makundi maalum kushiriki kwenye mnyororo wa thamani wa madini
-Yaongeza uzalishaji na kusambaza Rafiki Briquettes nchi nzima.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, ameipongeza STAMICO kwa juhudi zake za makusudi katika kupanua wigo wa wanufaika wa rasilimali za madini nchini, kwa kuanzisha na kutekeleza mikakati inayogusa makundi ambayo hapo awali hayakuwa sehemu ya moja kwa moja ya mnyororo wa thamani wa madini.
Akizungumza katika banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Dkt. Serera amesema kuwa hatua hiyo si tu kwamba inaongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa madini, bali pia inatoa fursa kwa watanzania wengi zaidi kunufaika na utajiri wa rasilimali hizo kwa njia mbalimbali.
“Niipongeze STAMICO kwa kuanza kushirikisha makundi maalumu ili kuonesha dira ya wazi ya kuhakikisha kuwa rasilimali za madini hazinufaishi tu wachimbaji au wawekezaji wa moja kwa moja, bali pia makundi mengine kama wanawake, vijana, kwani wangeweza kufanya kila kitu wenyewe” amesema Dkt. Serera.
Ameyaasa makundi ambayo yamepata fursa hizi katika nishati safi ya Rafiki Briquettes kuzingatia thamani ya bidhaa na kudhibiti bei ili iweze kumfikia kila Mtanzania kwa gharama nafuu
Aidha ameongeza kuwa sekta ya madini na sekta ya viwanda na biashara ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vya ndani vinavyotegemea malighafi kutoka kwenye sekta hiyo, hivyo mkakati wa kuiunganisha jamii kwa upana zaidi unapaswa kuungwa mkono na kuendelezwa kwa nguvu zaidi.
Kwa upande wa STAMICO Meneja wa Masoko na Uhusiano, Deus Alex amesema Shirika linaweka nguvu katika utunzaji wa mazingira kwa kuongeza uzalishaji wa nishati safi ya Rafiki Briquettes sambamba na kuendeleza miradi yake ya uchongaji, uchimbaji, Uchakataji uongezaji thamani na uuzaji wa Madini.
STAMICO imekuwa ikitekeleza Sera na mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa mafunzo, kusaidia wachimbaji wadogo kupata mikopo, kuendeleza masoko ya madini, pamoja na . Kushirikisha makundi maalumu yakiwemo ya Wanawake na Samia, hii imeleta mafanikio makubwa katika kuleta uwiano wa manufaa ya rasilimali za taifa kwa wananchi kwa ujumla.
Akiishukuru Wizara ya Madini kupitia STAMICO Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Dodoma, Fatuma Madidi amesema Wanawake wamekuwa wanufaika wa rasilimali madini kupitia bidhaa ya Rafiki Briquettes kwa kuwa imewapa fursa za kibiashara katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Geita, Njombe, Mbeya na Shinyanga.
Madidi amebainisha kuwa STAMICO imeshatoa uwakala kwa makundi ya Wanawake na Samia katika mikoa 26 na mikoa 7 imeshapatiwa kontena kwa ajili ya uuzaji wa nishati hiyo.
Hatua hiyo ya kuwajumuisha watu nje ya mnyororo wa kawaida wa uzalishaji wa madini imeelezwa kuwa ni ya kimkakati na muhimu katika kukuza uchumi jumuishi na wa watu wengi, sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kuwa rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wote.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...