Na Pamela Mollel,Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Labani Kihongosi, leo Alhamisi Agosti 21, 2025, ameungana na mamia ya wananchi wa Jiji la Arusha katika mazoezi ya viungo (Jogging) yaliyofanyika mapema alfajiri kama sehemu ya uzinduzi wa Tamasha la Tanzania Samia Connect.
Tamasha hilo, lililoanzishwa na Mhe. Kihongosi, linaadhimisha mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, sambamba na kutoa nafasi ya wananchi kushiriki katika shughuli za michezo, burudani na huduma mbalimbali muhimu.
Katika Viwanja vya Mgambo, Uzunguni Jijini Arusha, wananchi wanapata huduma bure ikiwemo vipimo na matibabu ya macho, uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, pamoja na ugawaji wa miwani zaidi ya elfu tatu kwa wahitaji. Huduma nyingine ni utoaji wa hati za ardhi, vitambulisho vya taifa na uraia, ukaguzi wa magari bila malipo, sambamba na huduma kutoka taasisi za serikali na sekta binafsi.
Aidha, tamasha hili limekuwa pia jukwaa la kuinua wajasiriamali wadogo kupitia mauzo ya bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula, vinywaji na kazi za mikono.
Tamasha la Tanzania Samia Connect litaendelea kwa siku tatu na litafikia kilele chake Agosti 23, 2025, likibaki kuwa kumbukumbu muhimu ya mshikamano wa wananchi wa Arusha katika kusherehekea mafanikio ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...