Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo ametembelea Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Awali katika ziara yake, Bw. Mombokaleo ametembelea Banda la Wizara ya Uchukuzi pamoja na mabanda ya taasisi zake zinazounda wizara hiyo.
Aidha, Bw. Mombokaleo ametembelea Banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa lengo la kupata ufahamu juu ya utendaji kazi wa mitambo ya kuzima moto katika majengo marefu ikumbukwe TAA inafanya kazi kwa ukaribu na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika viwanja vyake inavyosimamia
Katika banda la Mamlaka, Bw. Mombokaleo alipata maelezo juu ya elimu inayotolewa kwa Wadau wa Viwanja vya ndege pamoja na mrejesho kutoka kwa wadau ili kuangalia namna ya kuboresha zaidi shughuli za uendeshaji katika viwanja vya ndege.
Bw. Mombokaleo ameipongeza Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake kwa ushiriki wenye ubora na ubunifu katika maonesho haya, akisisitiza kuwa sekta ya uchukuzi ni mhimili muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kilimo, biashara na uwekezaji nchini.
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025", yakihimiza ushiriki wa wananchi na wadau katika maendeleo ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa tija. Maonesho haya yalianza rasmi Agosti 1, 2025 na yanatarajiwa kufungwa Agosti 8, 2025 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...