.jpeg)
Dar es Salaam
MWANAMITINDO nguli wa kimataifa, Miriam Odemba, amezindua kitabu chake kipya kinacholenga kuhamasisha maendeleo ya sekta ya mitindo na urembo nchini, huku akieleza dhamira yake ya kuwawezesha vijana na chipukizi kufanikisha ndoto zao katika tasnia hiyo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Miriam alisema kuwa kitabu hicho ni matokeo ya miaka mingi ya uzoefu na mafanikio katika anga za mitindo ya kimataifa, na kinawakilisha watu wote wanaoamini katika ubunifu na urembo.
"Ninapenda sana mitindo, na natamani wengi wapende na kufanikiwa zaidi kama mimi. Humu nimeweka wazi siri mbalimbali za kuwa juu katika urembo na mitindo. Ni hazina na faida kwa taifa zima," alisema Miriam.
Hafla hiyo ilihusisha pia tamasha maalum lililopewa jina la "Sauti ya Mitindo", lililowakutanisha mabingwa na chipukizi wa mitindo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Wadau wa sekta hiyo walijadili fursa na changamoto zinazokabili tasnia ya mitindo, urembo na fashion nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa BASATA, aliyeshindwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na majukumu maalum ya serikali, mwakilishi huyo alisema kuwa Katibu Mtendaji, Kedmond Mapana, alitamani sana kuwepo na alifuatilia kwa makini tukio hilo. Aidha, aliunga mkono juhudi za tamasha hilo akisema ni endelevu na ni hazina kwa Taifa katika tasnia ya urembo na mitindo.
"Ninamwakilisha Katibu Mtendaji, Kedmond Mapana, ambaye alitamani sana kuwepo leo, na anakupongeza sana Miriam kwa hatua hii kubwa. Anasema kuwa unaipeperusha vyema bendera ya nchi yetu kimataifa bila kuchoka, na sisi kama BASATA tumekuandalia kitu kizuri ambacho tutakitangaza kuanzia Jumatatu," alisema mwakilishi huyo.
Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) pia lilimpongeza Miriam kwa mchango wake mkubwa wa kuiwakilisha vyema Tanzania kimataifa na kuchochea mabadiliko chanya katika tasnia hiyo.
Katika tukio la kusisimua, binti mwenye umri wa miaka 11, Sofia, alishindwa kuzuia machozi baada ya kumpanda jukwaani kumshukuru Miriam kwa kumsaidia kuhudhuria hafla hiyo bila malipo.
"Nilimsikia Miriam akiongelea kuhusu tamasha la mitindo kwenye redio ya Clouds, katika kipindi cha ‘Leo Tena’. Niliguswa sana na kumwambia mama tumpigie simu. Mama yangu anajua kuwa ninapenda mitindo, na fedha pekee tuliyokuwa nayo ilikuwa ni shilingi elfu moja ya vocha. Baada ya mama kukubali na kumpigia Miriam, siamini kuwa leo hii nimehudhuria tukio hili la kipekee..." alishindwa kuendelea kusema na kuangusha machozi ya hisia.
Runway ya uzinduzi ilifanywa na vijana kutoka makundi maalum ya Salvation Army jijini Dar es Salaam, ikiwemo watoto waliojishughulisha na fashion show ya awali. Jukwaa hilo limepewa hadhi ya kimataifa, jambo lililowagusa wadau na kuchangia zaidi ya Shilingi milioni 1.2 kwa ajili ya mfuko wa kusaidia watu wenye mahitaji maalum.
Miriam amejulikana kwa jitihada zake katika kusaidia wasiojiweza, ikiwa ni pamoja na msaada wa karibuni kwa akina mama na watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa jumla, mamodeli 13 walishiriki kwenye runway hiyo, wakiwa wamevalia mavazi ya kipekee yaliyoundwa na wabunifu nguli nchini, wakiwemo wakufunzi kutoka Anna Collection, pamoja na ofisi za wabunifu maarufu Hamissa Mobetto Stylish na Mike Stylish.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...