Dar es Salaam, 13 Agosti 2025.
KAMPUNI ya Tanzania Breweries Plc (TBL) na PETPRO wameweka historia kwa kusaini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kuzindua mfumo wa kwanza wa kitaifa na unaoweza kuongeza ukusanyaji na urejelezaji wa chupa za kioo baada ya matumizi nchini Tanzania. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Makao Makuu ya TBL, Ilala, Dar es Salaam.
Ushirikiano huu wa kimkakati unakuja katika kipindi muhimu ambapo usimamizi wa taka za chupa za glasi na uhifadhi wa mazingira umekuwa miongoni mwa vipaumbele vikuu vya kitaifa. Mradi huu utashughulikia changamoto inayoendelea ya usimamizi wa taka za chupa za kioo baada ya matumizi, sambamba na kujenga suluhisho endelevu la muda mrefu litakalosaidia kulinda mazingira na kuimarisha uchumi.
Mfumo huu wa ushirikiano unalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha taka za chupa za glasi zinazotupwa dampo, kuongeza viwango vya uchakataji nchini, na kujenga uchumi kwa ongezeko la thamani katika mnyororo wa thamani nchini. Kwa kubadilisha taka za chupa ya glasi kuwa malighafi zenye thamani, mpango huu utachangia moja kwa moja katika kufanikisha malengo endelevu ya kitaifa kuendana na mkakati ramani endelevu wa TBL wa mwaka 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Bi. Michelle Kilpin, amesema:
"Ushirikiano huu na PETPRO ni mfano wa kuigwa kwa wazalishaji, unaowezesha uboreshaji wa uzalishaji, utunzaji wa mazingira na ukuaji wa uchumi. Tunafurahi kwa fursa hii inayotuwezesha kubadilisha taka za chupa ya glasi kuwa fursa, huku ikisaidia jamii husika na kulinda mazingira yetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Hatimaye, tunatarajia mpango huu kuwa jukwaa la kuimarisha uwajibikaji kwa wazalishaji ndani ya sekta, kupitia ushirikiano na wazalishaji wengine, tukitumia uwezo wa pamoja kufikia matokeo makubwa zaidi."
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PETPRO, Bw. Nicholaus Jackson,ameongeza kuwa:
"Kupitia ushirikiano huu na TBL, tunaweka mfano mpya wa kuchakata taka za chupa za glasi nchini Tanzania. Uzoefu wetu wa pamoja utahakikisha tunakusanya, tunachakata na mbinu endelevu zinazoleta matokeo chanya kwa uhifadhi wa mazingira na kutoa fursa za kiuchumi kwa Watanzania. Pamoja, tunajenga kesho iliyo safi na imara zaidi."
Zaidi ya manufaa ya kimazingira, mradi huu unatarajiwa kuleta fursa za kiuchumi kwa wakusanyaji taka, wachakataji, na wazalishaji kote nchini Tanzania. Kwa kuweka uhitaji endelevu wa chupa za glasi zilizochakatwa, mpango huu utasaidia kuzalisha kipato kwa maelfu ya watu wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa uchakataji, hususan katika jamii zenye uhitaji zaidi.
Utaalamu wa PETPRO katika uchakataji na usafirishaji, ukichanganywa na uzalishaji endelevu na mtandao mpana wa usambazaji wa TBL, utaiwezesha sekta kurejesha na kuchakata chupa za glasi kwa kiwango kikubwa. Aidha, ushirikiano huu utaweka msingi wa ushirikiano zaidi ndani ya sekta na kuwa mfano wa kuigwa na sekta nyingine, ukionyesha kuwa uwajibikaji wa mazingira na ukuaji wa biashara vinaweza kwenda sambamba.
Hati hii ya Makubaliano inathibitisha nafasi ya TBL na PETPRO kama waanzilishi katika mchakato wa Tanzania kuelekea uchumi wa mzunguko. Makampuni haya mawili yamejitolea kushirikiana kwa karibu na mashirika ya serikali, mamlaka za mitaa na wadau wa sekta ili kuboresha mfumo huu na kuupanua zaidi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...