Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tume na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 01, 2025.

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv 
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevihimiza vyombo vya habari nchini kuripoti kwa usahihi na kwa wakati kuhusu taarifa zote zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

Kauli hiyo imetolewa leo, tarehe 1 Agosti 2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati wa ufunguzi wa mkutano kati ya Tume na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Jaji Mwambegele amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya mpiga kura na taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi ya msingi kwa uhuru na kwa amani.

Aidha, amewasihi Wahariri wa vyombo vya habari kutumia majukwaa yao kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu, utakayofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Tume na vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kwa kuzingatia sheria za uchaguzi.

Akitoa mada kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima qmesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kufanikisha maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Ameongeza kuwa, katika nchi yoyote inayodhamiria kufanikisha jambo kubwa kama uchaguzi, vyombo vya habari ndio msingi wa kwanza, kwani kupitia kwao, wananchi hupata taarifa sahihi, zilizofanyiwa utafiti na kuhakikiwa.

Kailima amesema kuwa bila ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari, juhudi zote za Tume katika kutoa elimu na taarifa kwa umma haziwezi kuwafikia walengwa.

"Maana yake kila kinachotolewa na Tume hakiwezi kuwafikia wananchi iwapo vyombo vya habari havitaamua jambo hilo lifanikiwe," amesema.
Ameongeza kuwa wadau wote wa uchaguzi, vikiwemo vyama vya siasa, wanategemea vyombo vya habari kutoa taarifa zitakazowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

Amesisitiza kuwa vyombo vya habari ndivyo vinavyoweza kuwa sauti ya kwanza ya kuonesha upotoshwaji wa aina yoyote unaofanywa kwa bahati mbaya au kwa makusudi kuhusu Tume na kuhusu zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

“Tunawaomba na kuwanasihi, kutumia nafasi na fursa mlizonazo kuhakikisha kunakuwepo na taarifa za mara kwa mara za kuelezea kinachoendelea kuhusu uchaguzi,” amesisitiza Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Aidha, wahariri hao wamekumbushwa kutumia kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ambayo ni “Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura” kwenye taarifa zao wanazozitoa kwa umma ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji kwa wananchi kujitokeza kupiga kura.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) na Mhariri kutoka Clouds Media Group, Joyce Shebe, amesema waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati, hususan wakati huu ambapo nchi inaingia kwenye joto la Uchaguzi Mkuu.

Amesema, mkutano huo ni muhimu kwa kuwa unawapa wanahabari elimu sahihi kuhusu mchakato wa uchaguzi, ili hatimaye wao waweze kuielimisha jamii kwa usahihi.

"Elimu sahihi inasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi. Uwepo wetu hapa pamoja na Tume maana yake ni kwamba sisi kama wanahabari tunaenda kuelimika ili mwisho wa siku tuwaelimishe wananchi wapate elimu kwa wakati na wachague viongozi bora wa kuliongoza Taifa," alisema.

Naye, Salome Kitomari, Mhariri wa Gazeti la Nipashe, amesema mkutano huo umewapa nyenzo muhimu kama vile nakala za sheria za uchaguzi, kanuni, miongozo ya elimu ya mpiga kura na orodha ya taasisi zinazoelimisha na kuangalia uchaguzi. "Hii itatusaidia kupeleka taarifa sahihi kwa umma," alisema.

Kiondo Mshana, Mhariri wa Gazeti la Uhuru, amesisitiza umuhimu wa mafunzo ya mara kwa mara kwa wanahabari ili kuwajengea uelewa wa maadili ya uchaguzi na kuzuia taarifa zinazoweza kuchochea mtafaruku. "Tume inapaswa kutoa mafunzo haya mara kwa mara, siyo wakati wa uchaguzi pekee," ameeleza.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg Kailima Ramadhani akitoa mada wakati wa Kikao cha Tume na wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agost 01, 2025.

Sehemu ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakishiriki mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 01, 2025.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...