WAKULIMA 24 wa miti kutoka Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, wametembelea Kituo cha Mbegu za Miti Morogoro kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ili kujifunza mbinu bora za uandaaji wa vitalu na upandaji wa miti baada ya kukumbana na changamoto ya miche kutoota ipasavyo kwenye mashamba yao.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Greening Africa, unaotekelezwa na shirika la Prosper for Greening Africa Base Community, wenye lengo la kutunza mazingira, kurejesha uoto wa asili na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu wa mradi huo, Patrick Peter Monjare, alisema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima kwa kuwa yamewapa nafasi ya kuona kwa vitendo namna bora ya kuotesha na kutunza miche.
Kwa upande wake, Toribio Hullca Yabary, Mkurugenzi wa shirika hilo, alisema lengo la ziara hiyo limechochewa na changamoto kubwa iliyojitokeza baada ya kupandwa miti zaidi ya 380,000, ambapo takribani asilimia 30 ya miche haikuota vizuri na kusababisha wakulima kupata hasara.
“Tuliona ni vyema kuja kituo cha mbegu kujifunza njia bora za kuotesha miche na namna ya kuisafirisha ili kuipeleka shambani. Tunaamini elimu hii itasaidia kurejesha uoto wa asili na kutunza mazingira,” alisema Yabary.
Naye Mhifadhi Mwandamizi, Yahaya Saidi, ambaye ni Msimamizi wa Kituo cha Mbegu za Miti Morogoro, alisema ziara hiyo imekuwa fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu kati ya wataalamu wa kituo na wakulima.
“Waswahili husema kuona ni kuamini. Wakulima hawa wamepata nafasi ya kushuhudia namna mbegu bora zinavyotayarishwa, kuoteshwa na kuhamishiwa shambani. Tunatarajia ujuzi huu utawawezesha kuboresha miradi yao na kuongeza hamasa kwa vikundi vingine kuja kujifunza,” alisema Saidi.
Aidha, aliongeza kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana na wakulima kwa kuwapatia elimu ya vitendo, ikiwemo ziara za mashambani ili kushuhudia matokeo halisi ya matumizi ya mbegu bora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...