
Kivutio cha Mtwara
Na Mwandishi wetu, Mtwara
Wanajamii wilayani Mtwara vijijini wameahidi kuendelea na harakati za kupambana na ndoa za utotoni ili kumkomboa mtoto wa kike na kumuwezesha kwenda shule.
Wito huo umetolewa kijijini Nkunwa, wilayani Mtwara vijijini, leo wakati wakitoa maazimio ya kufunga mdahalo wa kijamii ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) pamoja na UN Women ili kujadili namna ya kutokomeza mila potofu na kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi.
Akiongea katika mdahalo huo, Mohamed Mponda amesema tangu wapate mafunzo kutoka TGNP wamekuwa wakitoa elimu kupitia redio jamii, shuleni, katika vikundi kama vikoba kwa kuelimisha makungwi , wanafunzi na wazazi ili kutoa elimu sahihi inayoendana na makuzi na hivyo kutokomeza ndoa za utotoni.
Kwa upande wake, mchungaji Sauli Mkulia amesema wao kama viongozi wa dini wamekuwa wakifuatilia kujua umri sahihi wa watoto kabla ya kufungisha ndoa na kuahidi kuendelea kufanya hivyo ili kutokomeza kabisa ndoa za utotoni.
“Tumekuwa tukitoa mafundisho ya dini katika nyumba za kuabudia na kukemea tabia ya kuoza watoto wadogo huku tukisisitiza wazazi kupeleka watoto shule,” amesema mchungaji huyo.
Asha Naumbu, mmoja wa washiriki wa mdahalo huo amesema wanawake wana uwezo wa kumiliki mali na kuwa viongozi iwapo tu watapata fursa ya kufanya hivyo.
“Hapo zamani, wanawake katika jamii yetu walikuwa hawaruhusiwi kumiliki chochote kwani walionekana kama hawana uwezo wowote. Kwa sasa, hali imeanza kubadilika baada ya mwamko wa mafunzo, “amesema Naumbu.
Mdahalo huo wa siku mbili umeshirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo walimu wa jando, makungwi, viongozi wa dini, wazee maarufu kwenye Jamii, maafisa maendelo ya jamii pamoja na wajumbe wa Vituo vya Taarifa na Maarifa.
TGNP kwa kushirikiana na UN Women kwa pamoja wanatekeleza mradi wa Wanawake na Uongozi pamoja na Haki za Kiuchumi katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...