
Meneja wa Frabby Tanzania Ltd, Alexander Vitaris,akisaini mkataba wakati wa hafla iliyowakutanisha waokaji wa keki hapa nchini. Kulia ni Meneja masoko, Usafirishaji na maendeleo ya biashara wa Kampuni ya Kerry Krater Mustafa Filiz.

KATIKA hatua ya kuimarisha ubora wa bidhaa za uokaji nchini, Frabby Tanzania Ltd, kwa kushirikiana na kampuni ya Davinci, imezindua rasmi bidhaa mpya ya Whipping Cream Powder, inayotarajiwa kuongeza tija na ubunifu kwa waokaji wa keki na vitafunwa mbalimbali nchini.
Uzinduzi wa bidhaa hiyo umefanyika sambamba na kusainiwa kwa mkataba wa usambazaji wa bidhaa za uokaji kati ya kampuni hizo mbili, ikiwa ni juhudi za pamoja kuimarisha upatikanaji wa malighafi bora kwa waokaji wa ndani.
Akizungumza Julai 31, 2025 wakati wa hafla hiyo, Meneja wa Frabby Tanzania Ltd, Alexander Vitaris, alisema Whipping Cream Powder ni suluhisho la kisasa kwa waokaji wa keki, hasa kwa mazingira yenye joto kama ya Tanzania, ambapo bidhaa hiyo hudumu muda mrefu na hutoa matokeo bora ya mapambo ya keki.
“Bidhaa hii ni tofauti na nyingine zilizopo sokoni. Ina kiwango kikubwa cha mafuta, iko katika mfumo wa unga, na inapopigwa hutoa uzito mzuri kwa ajili ya mapambo na ujazaji wa bidhaa za uokaji. Tunataka waokaji wa keki nchini wapate bidhaa bora kwa bei nafuu,” alisema Vitaris.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa bidhaa hiyo unaenda sambamba na mkakati mpana wa Frabby Tanzania Ltd kusambaza bidhaa zote muhimu kwa uokaji kupitia ushirikiano mpya na kampuni ya Davinci, inayotambulika kwa uzalishaji wa vinywaji vya Cocktail na Mocktail Syrups.
“Kupitia mkataba huu, tunalenga kuwawezesha waokaji wa keki kwa kuwapatia malighafi bora na zenye ubunifu. Sitawaangusha wadau wetu, nitakuwa karibu nao kwa mafunzo ya matumizi sahihi ya bidhaa hizi mpya,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa Tartan Pastries in Bakery, Joan Severine, alisema uzinduzi wa Whipping Cream Powder umekuja wakati muafaka ambapo waokaji wengi wanahitaji bidhaa bora na zenye ufanisi mkubwa.
“Nimefurahishwa na bidhaa hii. Inafaa sana kwa mazingira yetu ya joto na nipo tayari kuitumia katika keki na vitafunwa vyangu. Inavutia na inarahisisha kazi,” alisema Joan.
Alieleza kuwa Whipping Cream Powder itarahisisha kazi ya waokaji na kuongeza mvuto wa bidhaa zao kwa wateja, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara ndogondogo za uokaji nchini.
Uzinduzi wa bidhaa hiyo na ushirikiano kati ya Frabby Tanzania Ltd na Davinci ni ishara ya kuongezeka kwa ubunifu na uwekezaji katika sekta ya uokaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha viwanda vidogo na kuunga mkono ujasiriamali nchini.
Meneja masoko, Usafirishaji na maendeleo ya biashara wa Kampuni ya Kerry Krater Mustafa Filiz akizungumza mara baada ya kusaini mkataba na kampuni ya Frabby Tanzania Ltd.
Matukio mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...