Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma.
WAKATI zoezi la urejeshaji fomu limekamilika leo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,mgombea Urais kupitia tiketi ya ACT Luaga Mpina amezuiwa kuingia katika ofisi hizo kutokana na sababu mbalimbali.
Moja ya sababu zilizomfanya Mpina azuiwe getini ni kutokana na mgombea huyo kukosa vigezo vya kugombea nafasi hiyo ambapo moja ya kanuni ya chama hiko inamtaka mgombea wa nafasi hiyo awe amedumu ndani ya chama walau kwa siku 30.
Mpina ambaye aliwasili majira ya saa sita na dakika 40 mchana katika ofisi za INEC akiwa na mgombea mwenza alikutana na zuio hilo ambapo walimtaka kutokuingia ndani ya ofisi hizo.
Mpina pamoja na wanachama wa ACT walitakiwa kukaa nje ya ofisi za Tume ili wasubiri kama wataruhusiwa kuingia au la mwisho wa siku hawakuweza kuingia ndani ya ofisi za Tume kurejesha fomu hizo.
Chama hiko kiliwasili katika ofisi za Tume wakiwa na imani kurejesha fomu ili wajiandae kuanza kampeni katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
KUHUSU WAGOMBEA WA VYAMA VINGINE VYA SIASA.
Mgombea nafasi ya Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),DK Samia Suluhu Hassan DK Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza Dkt Emmanuel Nchimbi wamerejesha fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Rais Samia alichukua fomu hiyo Agosti 9 mwaka huu ambapo vyama vingine 17 navyo vilichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuongoza Nchi.
Vyama hivyo ni NRA,AAFP,Chama Makini,NLD,UPDP,ADA,TADEA,UMD,TLP,CCK,CHAUMA,DP,SAU,CUF,ADC,UDP,NCCR Mageuzi na UMD.
Mgombea huyo akiwa amesindikizwa na viongozi wa Chama hiko akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Stephen Wasira alifika katika ofisi za INEC zilizopo Njedengwa jijini Dodoma majira ya saa 7.50 asubuhi na kupokelewa na Mkurugenzi wa INEC,Ramadhan Kailima.
Mara baada ya kushuka katika gari akiwa na mgombea mwenza na baadhi ya viongozi wa CCM wakiwa wamevalia mavazi ya kijani wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Alhaj Adamu Kimbisa,alielekea ofsini kwa ajili ya zoezi la urejeshaji wa fomu.
Alitumia dakika 48 mpaka kukamilisha zoezi la urejeshaji fomu na baadae kutoka ndani ya ofisi hizo na kuzungumza kwa dakika chache na viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Katibu Mkuu wa CCM DK Asha Rose Migiro,Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Stephen Wasira pamoja na viongozi wengine wa chama hiko.
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taiga ya Uchaguzi (INEC),Ramadhan Kailima amesema wagombea hao waliopendekezwa wetimiza masharti ya Ibara ya 39 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,hivyo INEC imewateuwa wagombea hao wa CCM kuwania nafasi hizo kutokana na kukidhi vigezo.
Hata hivyo mgombea huyo amekabidhiwa gari aina ya Land Cruiser kwa ajili ya kampeni ambayo ataambatana nalo kuanzia leo mpaka kampeni zitakapoisha.
VYAMA VINASEMAJE KUHUSU KAMPENI
Wagombea Urais kupitia tiketi ya vyama mbalimbali vya siasa wameonyesha nyuso za furaha baada ya kukabidhiwa magari kwa ajili ya shughuli za kampeni zinazoanza rasmi kesho.
Mpaka sasa jumla ya wagombea 17 wamekidhi vigezo vya kuwania nafasi hizo za Urais na Makamu Urais kupitia tiketi za vyama vyao vya siasa.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele aliwaambia wagombea kuwa INEC itawakabidhi wagombea kila mmoja gari na dereva kwa ajili ya kampeni mpaka hapo watakapomaliza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa INEC Ramadhan Kailima alisema magari hayo yatatumiwa na wagombea katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Kailima alisema wagombea hao wamekabidhiwa magari na dereva kwa ajili ya kampeni huku akisema majina ya wagombea yamebandikwa kwenye ubao WA matangazo na kusisitiza uteuzi tayari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...